Ummy: NHIF walipeni watoa huduma ndani ya siku 30

Muktasari:

  • Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray alisema wamepunguza siku za malipo na kutoka siku 60 hadi 47.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwalipa watoa huduma za afya kwa wagonjwa ndani ya siku 30.

Sambamba na hilo, amesema ataangalia upya sheria ya mikataba ya malipo hayo ambayo inazitaka taasisi za bima kuwalipa ndani ya siku 60.

“Nimekuwa nikisema kila siku, iwalipe watoa huduma kwa wakati, sasa naagiza wafanye hivyo ndani ya siku 30,” alisema Ummy alipokuwa akizindua kliniki ya binafsi ya Hospitali ya CCBRT jana.

Alisema wanaotoa huduma wanategemea kujiendesha kwa fedha hizo, hivyo wanapolipwa ndani ya siku 60 inawawia vigumu.

Alisema mara zote walipaji wamekuwa wakijificha kwenye kisingizo cha kufanya uhakiki, “mnahakiki nini siku zote hizo? Walipeni ndani ya siku 30, wateja wenu huduma wamepata lakini mnawacheleweshea kwa nini?”

Aliwataka watoa huduma kuwasilisha maombi ya madai kwa wakati, ili kutoa nafasi kwa taratibu za malipo kufanyika mapema.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi alisema kwenye kliniki hiyo wateja wengi ni wale wanaotumia bima za afya.

“Changamoto ni kutolipwa kwa wakati jambo linalosababisha tupate wakati mgumu kwa sababu hizo fedha ndiyo tunazitegemea kujiendesha,” alisema Msangi.

Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray alisema wamepunguza siku za malipo na kutoka siku 60 hadi 47.

“Hatupingani na waziri, lakini tumebadili mambo mengi sana ikiwamo kupunguza siku za malipo. Taratibu nyingi zinafanyika kwa mtandao jambo ambalo linarahisisha kazi.

“Wakati mwingine changamoto ni wanaotuma maombi wanachelewa kuwasilisha, lakini tumepunguza sana siku, labda kwa malipo yenye matatizo yanayohitaji kujiridhisha,” alisema Mziray.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Tiba na Uchunguzi wa Maabara Tanzania (APHFTA), Dk Samwel Ogillo alisema NHIF wangekuwa wanalipa ndani ya siku 60 za kisheria isingekuwa na shida, lakini inafika hadi miezi sita.

“Kumekuwa na malalamiko mengi na tumeshafanya nao mikutano mingi na wamekuwa wakisema hawana wafanyakazi wa kutosha wanaajiri, hata walipoajiri pia mambo bado ni yale yale. Kuna maeneo ambayo kweli wanafanya kazi vizuri, lakini kwenye malipo mambo ni magumu mno waziri yupo sahihi wanapaswa kubadilika,” alisema Dk Ogillo.