Ummy Mwalimu aeleza mafanikio Serikali ya Tanzania kununua dawa kwa wazalishaji

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema tangu Serikali ianze kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka kwa wazalishaji imeokoa asilimia 40 ya fedha zilizokuwa zinatumika kwa mawakala

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema tangu Serikali ianze kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka kwa wazalishaji imeokoa asilimia 40 ya fedha zilizokuwa zinatumika kwa mawakala.

Akitoa mfano, amesema shuka moja lililokuwa likinunuliwa kwa Sh21,000, hivi sasa linanunuliwa kwa Sh11,200.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 18, 2019 katika mkutano wa tatu  wa wazalishaji na wasambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na mkutano wa pili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ajili ya kuokoa maisha kwa kusambaza huduma hiyo kwa ubora.

Waziri Ummy akieleza hali ilivyokuwa mwaka 2015 amesema, “Ndio tukaanza kununua kutoka kwa wazalishaji badala ya mawakala kwa kuwa na mikataba ya muda mrefu.”

Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wawekezaji  kuimarisha huduma za dawa nchini na kupunguza gharama kubwa inayotumika kuagiza dawa nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD),  Laurean Bwanakunu amesema mkutano huo unawezesha ushirikiano baina yao, wasambazaji na wazalishaji.

Amesema katika mkutano huo kuna wawekezaji na wazalishaji 150 kutoka nje na ndani ya nchi huku mkakati ukiwa kuwekeza katika viwanda vya ndani.

Naye mkurugenzi wa fedha na mipango wa MSD, Soko Mwakalobo amesema kuna viwanja katika Mikoa ya Mbeya, Mwanza na Kibaha kwa ajili ya kuwekeza viwanda vya dawa.