Under the Same Sun watoa kompyuta 21

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Under the same sun, Berthasia Ladslaus akikabidhi laptop kwa mmoja kati ya wanafunzi 21 wenye ualbino walionufaika na msaada huo

Muktasari:

Shirika la Under the Same Sun kupitia mfuko wake wa Vivian Grace Ash limetoa msaada wa kompyuta mpakato kwa wanafunzi 21 wenye ualbino

Dar es Salaam. Shirika la Under the Same Sun kupitia mfuko wake wa Vivian Grace Ash limetoa msaada wa kompyuta mpakato kwa wanafunzi 21 wenye ualbino kutoka vyuo mbalimbali nchini.

Kutolewa kwa kompyuta hizo kunafanya idadi ya wanufaika kufikia 53 ikiwa ni baada ya wanafunzi 13 kunufaika katika awamu ya kwanza na 19 katika awamu ya pili.

Akizungumza wakati akikabidhi kompyuta hizo,mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Berthasia Ladislaus amesema ugawaji komputa hizo unaenda sambamba na mafunzo ya siku tatu ili kuhakikisha kompyuta zinatumiwa kama zilivyokusudiwa.

 “Tunafanya hivyo kwa sababu tuna imani kuwa si wote wanafahamu matumizi ya kompyuta, ikiwa wanafahamu si sana na kuna wengine hawafahamu kabisa hivyo hatutaki kuwapatia kitu ambacho badala ya kuwa msaada iwe pambo bali kiongeze ufanisi katika kujifunza,” amesema Berthasia.

Amesema hadi kufikia awamu hii jumla ya Sh71 milioni zimetumika katika kufanikisha kila kitu ikiwemo mafunzo.

“Na hii ni kwa sababu shirika hili linatoa ufadhili wa kimasomo kwa wanafunzi wenye ualbino kwa asilimia 100 kwa sababu tunaamini wengine wanatoka katika familia duni hivyo ni ngumu baadhi ya vitu kumudu,” amesema Berthasia.

Sufian Ally ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya elimu ya watu wazima katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mnufaika wa kompyuta hizo amesema zimsaidia kukuza maandishi ambayo anaweza kuona ili asipate tabu wakati wa kujisomea.

“Baadhi ya walimu wamekuwa wakitoa notisi zenye maandishi madogo tusiyoweza kuona hivyo kupitia kompyuta hii nitakuwa nachukua katika flash, naongezea ukubwa na kuzichapisha katika karatasi,” amesema.