Upande wa utetezi kesi Jamii Forum waomba kufunga ushahidi

Muktasari:

Upande wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ufunge ushahidi katika  kesi ya kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini kwa kikoa cha .co .tz (Tanzania domain) inayomkabili, mkurugenzi mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo na Micke William.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ufunge ushahidi katika  kesi  ya kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini kwa kikoa cha .co .tz (Tanzania domain) inayomkabili mkurugenzi mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo na Micke William.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Daisy Makakala leo kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kuwa shahidi waliyekuwa wakimtegemea yupo nje ya mahakama hiyo na kuiomba Mahakama ipange tarehe fupi ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alisema mara nyingi shauri hilo likiwa linaahirisha kutokana na kutokuwapo kwa shahidi hivyo upande wa mashtaka hawatendei haki washtakiwa kwa kuwa lipo mahakamani hapo tangu mwaka 2016.

"Tunaiomba Mahakama hii ifunge ushahidi kila tunapokuja kwenye shauri hili tunaelezwa shahidi hayupo kinachotakiwa ni haki itendeke," alisema.

Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 18 mwaka huu itakapoendelea na ushahidi ambapo tayari mashahidi watano wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni, wilaya yaKinondoni.

Washtakiwa  wanadaiwa kuendesha mtandao ambayo haujasajiliwa nchini yaani .tz (Tanzania domain) na kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuzuia taarifa binafsi za wateja wa mtandao wake.