Upande wa utetezi kesi ya mchungaji kudaiwa kusafirisha heroin wamuangukia DPP

Muktasari:

Upande wa utetezi kesi ya kusafirisha  dawa za kulevya inayomkabili raia wa Nigeria, Mchungaji Henry Ogwuanyi na  wenzake wawili umeiomba ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuharakisha upelelezi

Dar es Salaam. Upande wa utetezi kesi ya kusafirisha  dawa za kulevya inayomkabili raia wa Nigeria, Mchungaji Henry Ogwuanyi na  wenzake wawili umeiomba ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuharakisha upelelezi.

Washitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni  Linde Mazure na Martin Blavie raia wa Nativian.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Mei 20, 2019 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya wakili wa Serikali, Faraji Nguka kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza shauri hilo.

Wakili wa Utetezi, Hassan Kiangio amedai ofisi ya DPP iharakishe upelelezi wa shauri hilo ili kesi iweze kuendelea mbele.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustine Rwezile ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 31, 2019 itakapotajwa tena huku washtakiwa wote wakirudishwa rumande.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa  kuwa Aprili 17, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walikutwa wakisafirisha kilo 4.87 za dawa za kulevya aina ya Heroin.