Upande wa utetezi mauaji ya mwanaharakati walia upelelezi kutokamilika

Muktasari:

Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya mwanaharakati  Wayne Lotter (52) umeutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya Wayne Lotter (52) umeutaka upande wa mashtaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefikia wapi kuhusu upelelezi wa kesi hiyo ya mauaji inayowakabili raia wa Burundi, Habonimana Nyandwi na wenzake 16.

Lotter alikuwa mkurugenzi na mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Palms Foundation, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selassie wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Leo Jumatano Januari 30, 2019 katika mahakama hiyo, upande wa utetezi umeibua hoja hiyo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Sada Mohammed amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Herman Lupogo  alidai kuwa mara ya mwisho upande wa mashataka ulidai mahakamani hapo kuwa upelelezi umekamilika wanasubiri kuwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

"Tumeona taarifa zinaenda mbele na kurudi nyuma, watuambie kama hawana uhakika watueleze kesi hii imefika katika hatua gani, tunataka tuelewe,"alidai Lupogo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 13, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Mbali na Nyandwi, washtakiwa wengine ni raia wa Burundi, Nduimana Jonas maarufu Mchungaji (40) mkazi wa Kamenge Burundi, Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A, Innocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana (31).

Wengine ni meneja wa Benki ya Barclays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B, Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala B na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi,  Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selassie iliyopo wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam wanadaiwa kumuua  Lotter.