Upelelezi kesi ya kigogo wa Takukuru unaendelea

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, ufuatiliaji na tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor umeeleza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, ufuatiliaji na tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor umeiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka nane likiwamo la utakatishaji wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh 1.477 bilioni.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo leo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa huyo  alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Machi 29 hivyo leo ni mara ya pili kesi hiyo imetajwa nwa kwamba bado wananaendelea na upelelezi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 25 na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Katika shtaka la kwanza la kughushi, inadaiwa tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018 akiwa makao makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa barua ya ofa ya kiwanja ikionyesha imetoka katika halmashauri ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Shtaka la pili, inadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 2012 na Mei 2017 akiwa eneo la Upanga, mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu  Sh 5.2 milioni kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Alex Mavika kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.

Katika shtaka la nane, ilidaiwa katika tarehe tofauti Januari mwaka 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh 1.477,243,000 huku akijua fedha hizo ni zao la makosa mengine.