Upinzani Kilimanjaro wawaka ujio wa makada CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo ambayo CCM kinajivunia ni utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiwatesa wananchi, kudhibiti  rushwa na nidhamu ya watumishi wa umma na kuboresha huduma za jamii.

Moshi. Ujio mfululizo wa viongozi wa kitaifa wa CCM katika mkoa wa Kilimanjaro, umewaibua viongozi wa upinzani wakiwamo wabunge, ambao wamedai ujio huo hautakisaidia chama hicho 2020.

Kauli za wabunge na viongozi wa upinzani unatokana na taarifa za viongozi hao wa CCM kuonekana kuushambulia zaidi mkoa wa Kilimanjaro unaoaminika kuwa ngome ya upinzani tangu 1995.

Miongoni mwa viongozi hao wa kitaifa ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally ambaye amekaririwa akisema wameshatesti mitambo na kubaini wala Kilimanjaro sio ngome ya upinzani.

Akiwa Jimbo la Hai linaloshikiliwa na Freeman Mbowe, Julai 7,2019 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne, Dk. Bashiru alisema jimbo la Hai na mkoa wa Kilimanjaro sio ngome ya upinzani.

Alisema kwa mara ya kwanza tangu ameteuliwa, Kilimanjaro ni Mkoa ameupangia siku nyingi kwenda wilaya kwa wilaya,kwa sababu ya uzito,umuhimu na umaalumu wa mkoa Kilimanjaro.

Mbali na Dk Bashiru, pia Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Polepole ndiye amefanya ziara nyingi kuliko kiongozi mwingine wa kitaifa, akipokea viongozi wa upinzani na wanachama wapya.

Viongozi wengine wa CCM waliofanya ziara katika mkoa huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James na Katibu mkuu wake, Raymond Magwala.

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Dk Edmund Mndolwa, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudensia Kabaka na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Jesca Mbogo.

Mbali na hao, wapo pia Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM (Nec) kupitia wazazi, Galila Wabanhu na Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vyuo vikuu nchini, Esther Mmasy.

Kote walikopita, viongozi hao wanadai kuridhika kuwa CCM sasa kinakubalika zaidi miongoni mwa wananchi kutokana na kukirudisha kuwa cha wananchi na kufanikiwa kutatua matatizo yao.

Miongoni mwa mambo ambayo CCM kinajivunia ni utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiwatesa wananchi, kudhibiti  rushwa na nidhamu ya watumishi wa umma na kuboresha huduma za jamii.

Mwenyekiti wa Madiwani wa CCM katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Priscus Tarimo, alisema ujio wa viongozi hao ni kielelezo kuwa CCM sasa ni wananchi.

"Wala (wapinzani) wasitafute visingizio. Kama Katibu mkuu wetu alivyosema mitambo imeshafungwa na imefanyiwa majaribio. Kilimanjaro inakwenda kuwa kijani 2020,"alisema.

Kwa mujibu wa Tarimo, alisema kwa miaka 20 ya upinzani katika baadhi ya majimbo, wananchi wameshajua pumba ni ipi na mchele ni upi na wabunge wao wanajua hawarudi.

Walichokisema wabunge wa upinzani

Mbunge wa Moshi mjini (Chadema), Jaffar Michael aliliambia gazeti hili miaka yote tangu 1995, CCM imekuwa ikijifariji kulitwaa jimbo la Moshi mjini na hawajahi kufanikiwa na 2020 itakuwa hivyo hivyo.

“Tutashinda kwa namna yoyote ile. Kama ni kazi tumefanya na wananchi wanaona. Kuanzia barabara, tumenunua magari ya takataka, tunajega stendi mpya na tumeboresha huduma za jamii,”alisema.

“Mimi kwa maoni yangu, Jimbo la Moshi mjini ndio litakuwa la kwanza kwa mgombea yeyote wa Chadema atakayeteuliwa kushinda nchini. Wananchi hawachagui rangi ya chama bali kazi,”alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu, naye kama ilivyo kwa Michael, alisema anaamini atarudi tena bungeni kwani anaamini hakuna jipya litakaloletwa na CCM likubalike.

“Wamekuja na vitisho ooh mkichagua upinzani hatutaleta maendeleo. Hebu angalia majimbo kama Mwanga na Same Magharibi si ndio yako nyuma zaidi hapa Kilimanjaro na ni ya CCM?”alihoji.

Komu alidai hali ya maisha kwa watanzania wengi sio nzuri, ukandamizaji ni mkubwa na suala la utekaji wa raia lililoibuka sasa linawakera watanzania na hilo ni moja ya mambo yatawaangusha.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, Katibu Mwenezi wa chama hicho taifa, Hemed Msabaha, alisema kati ya jimbo CCM watashindwa asubuhi ni Vunjo.

“Tunafahamu wamepita sana (viongozi wa kitaifa CCM) Kilimanjaro kufanya siasa. Wanafanya demokrasia ya upande mmoja.Waliruhusu mikutano ya vyama tucheze uwanja sawa,”alisema Msabaha.

“Wasiwe waoga. Kama wanajiamini wana uwezo wa kurejesha jimbo la Vunjo na majimbo mengine hapo Kilimanjaro basi waruhusu na wengine wacheze. Watupe fursa sawa tucheze waone,”alisisitiza.

Wabunge wa Hai, Freeman Mbowe, Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka na Rombo, Jopseph Seslasini wote kutoka Chadema hawakuweza kupatikana kwa kuwa sumu zao hazikupatikana.