Upitiaji mwenendo wa kesi wakwamisha kesi ya Mattaka

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili, kwa kile kilichoelezwa na upande wa utetezi kuwa bado hawajapitia mwenendo wa kesi hiyo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea, kwa kile kilichoelezwa na upande wa utetezi kuwa bado hawajapitia mwenendo wa kesi hiyo.

Mbali na Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk Ramadhan Mlinga na aliyekuwa mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni, linalomkabili Mattaka.

Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis amedai leo April 10, 2019, mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Rwezile kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya washtakiwa hao kujitetea baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

"Kesi imepangwa kwa ajili ya utetezi na upande wa mashtaka tuko tayari kusikiliza utetezi wa washtakiwa hawa," alidai Vitalis.

Baada ya Vitalis kueleza hayo, wakili anayewatetea washtakiwa hao, Peter Kibatala alidai kuwa walichelewa kupata mwenendo wa kesi hiyo.

" Tulipewa mwenendo wa kesi hii, April 5 mwaka huu wakati tukiwa jijini Arusha katika mkutano wa kumchagua Raisi wa Chama cha Mwanasheria nchini( TLS), hivyo hatukuweza kujiandaa kwa sababu tulikuwa bado hatujapitia mwenendo wa kesi hii," alidai Kibatala na kuongeza, "Kutokana na hali hii, tunaiomba  mahakama hii itupe siku chache ili tuweze kupitia mwenendo wa shauri hili."

Hakimu Rwezile baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 10, mwaka huu itakapokuja kwa washtakiwa hao kuanza kujitetea na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Tayari mashahidi 18 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hao, ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo Paul Kimiti (73) ambaye alidai kuwa aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa ujumbe wa bodi ya ATCL, baada ya kubaini kuwa menejimenti ya shirika hilo, ilikuwa inakodi ndege bila kufuata utaratibu.

Alidai menejimenti ya ATCL ilifanya uamuzi mbaya wa kukodi ndege bila kuishirikisha bodi, jambo lililosababisha hasara kwa Serikali.

Katika ushahidi wake, Kimiti alidai kuwa aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya ATCL, mwaka 2007, lakini ilipofika mwaka 2009, aliamua kujiuzulu nafasi yake, kutokana na menejiment ya ATCL kukodi ndege aina ya Airbus 320-214 kutoka kampuni ya Wallis Trading, bila kuishirikisha bodi ya ATCL.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mattaka, anadaiwa kuwa Oktoba 9, 2007, wakati akitekeleza majukumu yake kama Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus na kwamba mkataba huo unadaiwa  kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 71bilioni.

Katika shtaka la kughushi, linalomkabili Dk Mlinga na Soka, inadawa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA zilizopo wilaya ya Ilala, washtakiwa walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionyesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL kukodisha ndege, wakati wakijua kuwa ni uongo.