Usafiri chanzo Sethi, Rugemalira kutofikishwa mahakamani

Thursday November 22 2018

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Washtakiwa Harbinder Seth na mfanyabiashara James  Rugemalira  leo Alhamisi Novemba 22, 2018 wameshindwa kufikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu ya shida ya usafiri.

Hayo yameelezwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Wawili hao wanakabiliwa na  mashtaka 12 ya uhujumu uchumi ikiwamo ya utakatishaji wa fedha.

Wakili wa Serikali Emmanuel Nitume amesema mahakamani kuwa washtakiwa wote wanaokabiliwa na kesi hiyo hawapo kwa sababu kuna shida ya kusafiri.

Wakati Nitume akieleza hayo, ofisa mmoja wa Jeshi la Magereza aliyekuwepo mahakamani hapo alisisitiza jambo hilo la shida ya usafiri.

Katika maelezo yake Nitume amedai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado unaendelea na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi  Desemba 6, 2018.

Washtakiwa hao  wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya Dola 22milioni za Marekani na Sh 309,461,300,158.27.

Wakati hayo yakielezwa mahakamani walikuwepo mawakili wa utetezi, Dollah Mallaba na Kamala Stephano na ndugu, jamaa na familia za washtakiwa hao.

Soma zaidi:


Advertisement