Usaili JKT waibua tishio homa ya ini mkoani Mtwara

Wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Mtwara (RCC) wakiendelea na kikao. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

Vijana 12 wa Mkoa wa Mtwara wamekosa sifa ya kujiunga na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) baada ya kubainika kuwa na ugonjwa wa homa ya ini

Mtwara. Vijana 12 wa Mkoa wa Mtwara wamekosa sifa ya kujiunga na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) baada ya kubainika kuwa na ugonjwa wa homa ya ini.

Wamebainika katika usaili wa kujiunga na jeshi hilo baada ya kupimwa.

Akizungumza leo Jumatano Julai 17,2019 katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC), mkuu wa Mkoa wa Mtwara,   Gelasius Byakanwa amesema wakati wa usaili kuna taarifa zinaonyesha viashiria vya uwepo wa ugonjwa wa homa ya ini mkoani humo.

Amesema kati ya vijana 325, 12 wameshindw akujiunga na JKT baada ya kukutwa na ugonjwa huo ambapo asilimia kubwa wanatoka katika wilaya ya Nanyumbu.

“Tumeamua vijana hao wasirudishwe kwenye jamii kwanza na RMO (mganga mkuu wa mkoa) atabidi akutane nao tujue pengine huu ugonjwa uko katika hali gani lakini tuanze kuchukua tahadhari mapema,” amesema Byakanwa.

Amefafanua vijana kumi kati ya 12 wanatoka katika wilaya ya Nanyumbu na wawili ni Wilaya ya Newala na kuwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara hususani ugonjwa wa homa ya ini na kujua hali zao.