Ushahidi kesi ya Zitto kuanza kutolewa Januari 29

Monday January 14 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imepanga Januari 29, 2019, kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe anayekabiliwa na kesi ya uchochezi.

Mbunge huyo alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Januari 14, 2019 na Hakimu Mkazi, Janeth Mtega wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali Adolf Kissima amedai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka hawana jalada halisi la kesi hiyo.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka hatuna jalada halisi la kesi hii hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Kissima.

Kissima baada ya kueleza hayo, Wakili wa Zitto, Steven Mwakibolwa aliikumbusha mahakama kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na mahakama hiyo ilishapanga tarehe ya kuanza kusikilizwa, ambayo ni Januari 29, 2019.

"Kwa kumkumbusha msomi mwenzangu (Wakili Kissima) kuwa shauri hili lilishapangwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hii, Huruma Shaidi, kuwa Januari 29, 2019, litaanza kusikilizwa, hivyo tunaiomba mahakama hii ipange tarehe hiyo kwa ajili ya usikilizwaji na si kutajwa" amedai Mwakibolwa.

Baada ya kusikilizwa hoja za pande zote, Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, 2019 itakapoanza kusikilizwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

 

Katika kesi ya msingi,  Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo,  Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za  makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa kuwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua"

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa ni maneno ambayo ni ya uchochezi yenye kuleta hisia za hofu na chuki.

Advertisement