Ushindani urais bado ngoma nzito

Thursday November 13 2014

By Nuzulack Dausen, Mwananchi

Dar es Salaam. Kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete bado ni kigumu kutokana na Watanzania wengi kushindwa kubainisha ni mwanasiasa gani wangemchagua kwa wingi iwapo angegombea urais mwaka 2015.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya Twaweza iliyotolewa jana, mtu mmoja kati ya watatu (asilimia 33), walisema hawajaamua na kwamba uwanja huo wa ushindani huenda ukawa mpana zaidi iwapo mgombea muhimu wa CCM atajiondoa kwenye chama na kwenda upinzani.

“Mtu mmoja kati ya wapigakura watatu alijibu kuwa hajui wa kumchagua idadi ambayo ni karibu sawa na asilimia za wagombea watatu wenye alama za juu zikichanganywa pamoja.

“Hii inaonyesha kuwa kinyang’anyiro cha urais kiko wazi zaidi, kwa maana kwamba Watanzania bado hawajashawishika vya kutosha na wagombea waliojitangaza,” inasema ripoti hiyo iliyowasilishwa na mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Pamoja na kwamba wengi bado hawajaamua, wapigakura wa mwaka huu kati ya watu 1,445, wanampenda zaidi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa asilimia 13, Waziri Mkuu Mizengo Pinda (asilimia 12) wote wa CCM na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa asilimia kumi na moja.

Pia, wamo viongozi wengine waliotajwa kuwa wangechaguliwa na zaidi ya asilimia tano ya waliohojiwa ambao ni mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwa asilimia sita na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kwa asilimia tano.

Advertisement

Watafitiwa hao ambao waliulizwa iwapo uchaguzi ungefanyika leo wangemchagua nani kama mtu huyo angekuwa mgombea, pia waliwataja viongozi wengine, ambao ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwa asilimia nne na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kwa asilimia tatu,

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye alipigiwa kura kwa asilimia tatu wakati mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe akipata asilimia moja ya watu waliohojiwa.

“Kwa maana hiyo, upenzi wa chama una uwezekano wa kuchangia sana kuamua nani mshindi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo na kubainisha kuondoka kwa mgombea muhimu ndani ya CCM na kujiunga upinzani, kunaweza kupanua wigo wa ushindani.

Advertisement