Uswisi wamwaga mabilioni kwa asasi za kiraia

Muktasari:

Ubalozi wa Uswisi nchini umetoa Sh18 bilioni kwa asasi za kiraia ili zitumike katika kuhamasisha uwajibikaji wa mamlaka za umma. Fedha hizo ni kwa ajili ya awamu ya tatu ya program ya uwajibikaji wa kijamii.

Dar es Salaam. Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kupitia Shirika lake la maendeleo la SDC umetoa Sh18 bilioni kwa Asasi za Kiraia (Azaki) ili zifanye kazi ya kuimarisha utendaji na kuboresha uwajibikaji wa mamlaka za umma nchini.

Fedha hizo zimetolewa kwa asasi tatu za Foundation for Civil Society, Policy Forum na Taasisi ya Twaweza kwa kipindi cha miaka minne. Asasi hizo nazo zitatoa fedha kwa asasi ndogondogo zinazofanya kazi ya kuhamasisha uwajibikaji hapa nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano hayo leo Ijumaa Machi 22, 2019  jijini Dar es Salaam, Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli amesema nchi yake imejizatiti  kuwezesha uwajibikaji wa mamlaka za umma ili zitoe huduma bora kwa wanawake, wanaume na vijana hapa Tanzania.

“Tunajisikia fahari kufanya kazi na asasi za kiraia kwa sababu ni wadau wa sera wanaofanya kazi ya kuboresha maisha ya Watanzania wa kawaida,” amesema Mattli na kuongeza kuwa anaamini asasi za kiraia zenye nguvu ni chachu ya maendeleo ya Tanzania ili kufika malengo ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Amezitaka taasisi za serikali za uwajibikaji kama vile Taasisi la Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iongeze uwezo wa kufanya uchunguzi na kusimamia matumizi bora ya fedha kwa maendeleo ya wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema kuna misingi mitatu ya utawala bora ambayo ni uwazi katika utekelezaji wa miradi, umuhimu wa kushirikisha wananchi na uwajibikaji wa mamlaka za Serikali na wananchi kwa ujumla.

Eyakuze amesema kupitia msaada huo kutoka Serikali ya Uswisi, wataweza kuwasilisha mawazo ya wananchi na Serikali kupitia vyombo vyake vya uwajibikaji kuchukua hatua pale inapobainika hakuna uwajibikaji wa watendaji katika ofisi za umma.

“Tunaishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada huu, tunawahakikishia kwamba tutafanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya. Matatizo sugu kama vile umaskini, ujinga na maradhi bado yapo, tusipokuwa wabunifu yataendelea kuwepo siku zote,” amesema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa bodi ya Policy Forum, Japhet Makongo amesema asasi yao ina mtandao wa asasi 79 hapa nchini ambazo kwa pamoja zinafanya kazi ya kuhamasisha uwajibikaji kwenye matumizi ya rasilimali za umma.

“Nasi pia tunaahidi kutumia msaada huu katika kusimamia uwajibikaji wa rasilimali za umma. Tutashirikiana na wenzetu katika kutimiza malengo ya kazi yetu,” amesema mwenyekiti huyo wa bodi.