Utafiti : Wakenya wengi wana amini Kenyatta hawezi vita dhidi ya ufisadi

Wednesday March 6 2019

 

Nairobi, Kenya. Watu wawili katika kila watatu nchini Kenya (theluthi mbili) wana amini Rais Uhuru Kenyatta hawezi kupambana na ufisadi nchini humo.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Utafiti la Twaweza nchini humo inaonyesha Wakenya wengi wana amini vita hivyo havitafanikiwa kwani baadhi ya viongozi wa Serikali wanahusika kwenye matukio kadhaa ya ufisadi.

Akitoa ripoti hiyo, Mtafiti Mkuu wa Twaweza Kenya, Victor Rateng’ alisema wananchi wengi wanaamini ufisadi mkubwa unafanywa na viongozi.

Utafiti huo unajiri wakati viongozi mbalimbali wanaendelea kulaumiana kuhusu sakata la ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet ambako inaaminika huenda Sh21 bilioni zimeliwa.

Sakata jingine ambalo limeikumba Serikali ni kupotea kwa Sh1.6 bilioni katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS), Wizara ya Afya ambapo zaidi ya Sh5 bilioni zinaaminika kufujwa.

Licha ya hayo, Rais Kenyatta ameapa kukabiliana na tatizo  hilo akiiagiza ofisi ya mkurugenzi wa  makosa ya jinai (DCI), George Kinoti, mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP), Noordin Haji na mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Twalib Mbarak kuwakabili vikali wahusika.

Theluthi  moja ya Wakenya ilitaja ufisadi kuwa changamoto kuu iliyoiathiri nchi kwa mwaka mmoja uliopita. Wengi walikubali kupokea rushwa  au kukubali kutoa ili kupata huduma mbalimbali kutoka asasi za umma.

Utafiti vilevile ulionyesha kwamba theluthi  mbili ya Wakenya wanataja hali ngumu ya maisha kama changamoto kuu zinazowaathiri kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa kuu za kimsingi kama vyakula.

Hata hivyo, baadhi walieleza kuridhishwa na juhudi za Serikali katika sekta za elimu, kuimarisha usalama na usambazaji wa umeme.

“Wengi wanasifia juhudi hizo, wakieleza zinachangia sana katika kuimarisha maisha yao kwa kuwawezesha kubuni ajira zaidi,” alisema

Serikali imekuwa ikiwekeza sehemu kubwa ya sekta ya elimu, baadhi ya malengo makuu yakiwa utekelezaji wa mfumo mpya wa 2-6-6-3.

Kamati ya bunge yasimamisha miradi

Kamati ya Bunge ya Mazingira na Mali Asili nchini humo ilisitisha miradi ya thamani ya Sh188 bilioni ambayo zabuni yake haijatolewa na Serikali.

“Kamati hii inaamuru kusimamishwa kwa utekelezaji wa miradi yote ya ujenzi wa mabwawa na ambayo zabuni hazijatolewa hadi pale mipango ya ulipaji ridhaa ya wenye ardhi itakapokamilishwa na pesa hizo kutolewa.

”Serikali ipate ardhi kwanza kubla ya kuomba mikopo ya ufadhili wa miradi kama hiyo,” alisema  Kareke Mbuiki ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo.

 

 


Advertisement