VIDEO: Utata zaidi waibuka aliyejirusha ghorofani

Mwanza. Bado utata. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu tukio la mtu asiyejulikana aliyekutwa amekufa nje ya eneo la Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza baada ya kamera za ulinzi (CCTV) kuonyesha alijirusha kutoka ghorofa ya nne ya hoteli hiyo.

Msimamizi wa idara ya ulinzi wa jengo la hoteli hiyo yenye ghorofa kumi, Benard Kakongo alizungumza na Mwananchi jana na kubainisha kuwa hakuna kamera iliyomnasa mtu huyo wakati akiingia eneo hilo.

“Tumeshakabidhi picha zilizonasa tukio hilo kwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kakongo.

Akijibu swali kwa nini kamera hizo zinase tukio la kujirusha pekee bila kuonyesha mtu huyo akiingia, alisema inawezekana alitumia njia ya kuingia magari au ile ya wafanyakazi ambayo haikuwa na kamera za ulinzi.

Hoteli ya Gold Crest iko katika jengo linalomilikiwa na uliokuwa Mfuko wa Pensheni wa PPF katika makutano ya barabara za Kenyatta na Posta jijini Mwanza.

Eneo ulikokutwa mwili wa mtu huyo mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 unatazamana na kituo cha mafuta cha Puma na ofisi kadhaa za binafsi na umma zikiwemo za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Takukuru) Mwanza.

Anayeingia hotelini hapo hulazimika kutumia ama mlango mkuu wenye mitambo na mashine maalumu za usalama inayolindwa kwa saa 24 au njia ya magari ambayo pia kwa mujibu wa Kakongo pia hutumiwa na wafanyakazi wakati wa kuingia na kutoka kazini.

Tofauti na lango kuu, njia hiyo ya magari na watumishi haina mitambo, mashine ya ulinzi wala ukaguzi wa wanaoingia na kutoka.

“Watu wote wanaoingia na kutoka kupitia lango kuu hukaguliwa kwa mashine maalumu na kunaswa na kamera za ulinzi ambazo pia huchukua matukio yote yanayotokea kuzunguka jengo isipokuwa njia ya kuingia na kutoka magari,” alisema Kakongo.

Kakongo alisema uchunguzi wa kina umebaini kuwa mtu huyo hakuwa mmoja wa wapangaji wala wateja wa hoteli hiyo.

“Hadi sasa hakuna aliyefika hapa (hotelini) kumuulizia mtu huyo, labda kama wameenda huko polisi,” alieleza Kakongo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro aliwaeleza wanahabari juzi kuwa uchunguzi wa awali wa mwili wa marehemu na kwenye eneo la tukio linafifisha madai ya mtu huyo kujirusha.

“Mwili wa marehemu haukukutwa na jeraha lolote la kuvunjika wala kupasuka; hata eneo alilokutwa hakukuwa na damu. Hii inaondoa uvumi kuwa alijirusha kutoka ghorofani kwa sababu siyo rahisi mtu kujirusha kutoka ghorofa ya nne asivunjike wala kuvuja damu,” alisema Kamanda Muliro alipojibu taarifa za marehemu kudaiwa kujirusha.

Jana Mwananchi lilimtafuta Kamanda Muliro bila mafanikio kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa huku taarifa zikieleza kuwa alikuwa katika hafla ya kupokea Mwenge wa Uhuru mkoani Mwanza.