Utenguzi, uteuzi waacha furaha, majonzi Ruvuma

Dar/ Ruvuma. Ziara ya Rais Magufuli imehitimishwa mkoani Ruvuma ikimuacha mteule wake mmoja akiumia, huku mwingine akifurahi.

Hatua ya wateule hao wawili ambao siku ya jana kwao ilimalizika wakiwa katika ‘anga’ tofauti ilikuja baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Nyasa mkoani humo, Dk Oscar Mbyuzi na kutangaza kumteua katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Jimson Mhagama kuwa mkurugenzi mpya.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutenguliwa, Mbyuzi alisema ameumia moyoni, lakini ameupokea utenguzi huo kwa sababu umetolewa na aliyempa dhamana hiyo.

“Nimepewa taarifa (ya kutenguliwa) na nimepokea ingawa nimeumia, ila mwenye dhamana ndiye ameamua, tuishie hapo,” alisema kwa ufupi.

Naye Mhagama alisema, “nashukuru kwa kuteuliwa.”

Ingawa taarifa ya kurugenzi ya mawasiliano ya Rais (Ikulu) haikueleza sababu za utenguzi na uteuzi huo, hata hivyo unaweza kuwa na uhusiano na ziara ya Rais inayoendelea mikoa ya kusini iliyoanzia Mtwara mwanzoni mwa wiki.

Fedha za wahisani

Akiwa ziarani Madaba mkoani humo, Rais Magufuli alitaja sababu za kupeleka fedha za wahisani moja kwa moja kwenye miradi ya wananchi kuwa inatokana na kutumiwa vibaya na baadhi ya watendaji.

Rais alisema alipokuwa akizindua Kituo cha Afya Madaba kuwa, baada ya fedha za wadau kutumiwa vibaya kila zinapotolewa waliamua ziwe zinapelekwa moja kwa moja kwenye miradi husika.

“Lazima tuseme kweli. Siyo kwamba wafadhili wetu walikuwa hawatoi fedha za afya, siku za nyuma walikuwa wakitoa lakini watendaji wetu katika halmashauri walikuwa wakizitafuna, lakini sasa tumeamua fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwenye zahanati au kituo cha afya,” alisema.

Rais Magufuli alijivunia kuwa na mawaziri na watendaji wazuri wa wizara za Afya na Tamisemi.

“Nitumie nafasi hii kuwaambia watendaji wa Wizara ya Afya na Tamisemi kuendelea na tabia ya kusimamia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo.”

Alisema, “nawataka wakurugenzi na watendaji wa halmashauri kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa ajili ya masuala ya afya zinatumika ipasavyo.”

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wananchi wa Madaba kuanzia sasa hawatasumbuka kusafiri kilomita 100 kufuata huduma ya upasuaji ya uzazi mjini Songea, bali watafanyiwa kwenye kituo chao cha afya.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege alisema Sh650 milioni zimetumika kwenye ujenzi wa kituo hicho, kati ya fedha hizo Sh220 milioni zilinunua vifaa.

Uzinduzi kiwanda Njombe

Akizindua kiwanda cha kuchakata majani ya chai mabichi cha Kabambe, kilichopo Njombe mjini, Rais Magufuli alisema ni vyema mawaziri wa Fedha na Mipango, Kilimo pamoja na Viwanda na Biashara wakashirikiana na wabunge kuangalia namna watakavyowasaidia wananchi na wawekezaji.

Rais Magufuli alikubaliana na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook aliyesema kuwa kuna changamoto katika uwekezaji, hali inayosabababisha wanaotaka kuwekeza kuachana na mpango huo. “Mtu akitaka kuwekeza anapata shida na masharti ya ajabu ajabu. Nakubaliana na (balozi) Cook kuwa baadhi ya watendaji wa Serikali ni matatizo katika masuala ya uwekezaji,” alisema Rais Magufuli.

“Wanamuona mwekezaji kama adui, badala ya rafiki. Watendaji wabadilike, mtu anataka kuwekeza kiwanda lakini anazungushwa mwaka mzima, watu wetu wamekuwa na vichwa vigumu nafuu vya kamongo, hawataki kuelewa.”

Kamongo ni samaki jamii ya kambale.

Rais alifafanua kuwa kuna baadhi ya wawekezaji waliofika nchini lakini waliwekewa mikwara na kuamua kutimkia nchi za jirani, huku wengine wakiombwa rushwa ili mipango yao ya kuwekeza ifanikiwe.

“Mtu akija leo anataka kuwekeza apewa eneo ili kesho aanze kazi. Narudi hapa mwekezaji yeyote akipata ardhi aanze kujenga asihangaike na mambo mengine, anza nasema mimi sasa kwa sababu ndio Rais, tunachelewa,” alisema.