Utulivu warejea eneo la Gaza

Muktasari:

  • Shughuli zaendelea, reli yaanza kazi, benki shule nazo zaanza kutoa huduma kwa wananchi

Gaza, Palestina. Mara tu baada ya Jeshi la Israel kuondoa vizuizi karibu na eneo la Gaza baada ya mpango wa kusitisha mapigano kufikiwa ili kumaliza mapigano ya tangu 2014 kati ya nchi hiyo na kundi linalotawala Gaza la Hamas, hali ya utulivu imerejea na shughuli kuendelea kama kawaida.

Wizara ya Usafiri ya Israel imetangaza kuwa usafiri wote wa umma katika eneo la kusini mwa nchi hiyo utarejea na shughuli zitaendelea kama kawaida.

Njia ya reli kati ya miji ya Ashkelon na Beersheba ilitarajiwa kuanza kutumika tena leo asubuhi.

Vilevile, benki kwenye eneo hilo tayari zimefunguliwa baada ya kufungwa kwa siku tatu na shule zimefunguliwa leo.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amesema wapatanishi wa Misri wakisaidiana na wajumbe kutoka Qatar na Umoja wa Mataifa wamefanikisha makubaliano hayo ili kutuliza hali iliyokuwapo awali.

''Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza baada ya wapatanishi kuingilia kati na tunaliangalia hili suala la kuyakalia maeneo jinsi linavyoendelea, tuko tayari kujibu mashambulizi iwapo utafanyika uchokozi wa aina yoyote ile. Suala la ukaliaji (maeneo) ni lazima liendane na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na pande zinazohasimiana,'' amesema Qassem akinukuliwa na Sauti ya Ujerumani.

Mapigano hayo ya siku mbili yamewaua watu 23 kwa upande wa Gaza, wakiwemo wapiganaji na raia, huku kwa upande wa Israel raia wawili wameuawa.

Kundi la Hamas linaloitawala Gaza na ambalo Israel inalishutumu kwa kuchochea ghasia za sasa, limethibitisha kwamba makubaliano yamefikiwa chini ya usimamizi wa Misri. Miongoni mwa waliouawa ni wapiganaji tisa, wanawake wawili wajawazito na watoto wawili.

Mashambulizi yalianza mwishoni mwa wiki

Qassem amesema mashambulizi yalianza Jumamosi kutoka Gaza, na Israel ikarusha makombora ya kujibu na mashambulizi hayo yakaendelea hadi jana Jumapili.

Wapiganaji wa Kipalestina walifyatua mamia ya maroketi kuelekea Israel, huku jeshi la Israel likijibu mashambulizi katika maeneo yapatayo 350 ya wapiganaji ndani ya Gaza.

Maeneo yaliyolengwa na Israel ni pamoja na maghala ya kuhifadhia silaha, mahandaki pamoja na maeneo ya kutengeneza maroketi.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema  operesheni bado haijamalizika na inahitaji uvumilivu zaidi. Israel na Hamas wamekuwa maadui wakubwa na wamepigana vita vya miaka mitatu na mashambulizi mengine madogomadogo tangu kundi hilo la jihadi lilipoidhibiti Gaza mwaka 2017.