Uvuvi wa mabomu unavyoendelea kutafuna wengi

Baada ya operesheni kali ya kutokomeza uvuvi wa mabomu katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi, madhara ya uvuvi huo haramu yanaendelea kutesa wengi licha ya ahueni kidogo kuanza kuonekana.

Miaka mitatu iliyopita uvuvi huo ulikuwa umeshamiri katika ukanda huo baada ya baadhi ya wavuvi kuamua kutumia vilipuzi baharini kinyume na utaratibu ili kupata samaki wengi na hivyo kujiongeza kipato.

Jambo ambalo wengi walikuwa hawafahamu ni kwamba mbali na vitendo hivyo kuathiri afya na mazingira, uvuvi huo umeendelea kuzitafuna sekta nyinginezo zinazotegemea mazao ya bahari kama utalii na biashara huku baadhi ya wavuvi wakibaki vilema.

Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa habari wa Nukta, umebaini kuwa licha ya Serikali kudhibiti uvuvi huo kwa asilimia 85, kiwango cha upatikanaji samaki bado hakijaimarika kama awali, bei ya vitoweo hivyo ipo juu kutokana na kuadimika sokoni na wakati mwingine wafanyabiashara wanahaha kupata wateja.

Baadhi ya wavuvi wameeleza kuwa uvuvi wa mabomu umesababisha samaki kutopatikana kwa wingi huku aina nyingine za samaki zikipatikana kwa nadra akiwemo sehewa ambaye huenda sasa akapatikana mara moja kwa mwaka.

Ramadhan Almasi (40) mvuvi wa kijiji cha uvuvi cha Minazi Mikinda jijini Dar es Salaam, anasema kwa sasa kumpata samaki aina ya kolekole ni kama “kuokota almasi”.

“samaki aina ya bunusi ambao hupendelea sehemu iliyotulia, tangu wavuvi waanze kutumia mabomu wamejisogeza mbali,” anasema Almasi ambaye amekuwa akifanya shughuli za uvuvi kwa miaka 21 sasa.

Muuza samaki wa Mbagala Rangi Tatu, Richard Mmbaga (32) aliyefanya biashara kwa miaka mitano sasa, anasema jodari, changu, kolekole na vibua ni samaki wanao patikana “kwa manati kwa sasa”.

Uhaba huo umesababisha biashara ya samaki kutofanya vyema ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wa ukanda wa Pwani hutegemea sekta hiyo kujiingizia kipato.

Baadhi ya wachuuzi wameeleza kuwa wananunua samaki wanaovuliwa kutoka nje ya nchi wakiwemo vibua ili kumudu mahitaji.

“Samaki wangekuwepo, ungekuta hili soko limechangamka. Sasa hivi samaki hamna ndiyo maana unaona kupo kimya,” anasema Ali Waziri (48) mvuvi na mkazi wa Kunduchi.

Wakati wanahabari wetu wanatembelea soko la Kunduchi mwishoni mwa Septemba mwaka huu, walikuta kinamama wamekalia ndoo zao pasi na matumaini ya kupata samaki wa kwenda kuuza kwenye vijiwe vyao.

Kutokana na ukosefu wa samaki uliochochewa na kuharibiwa kwa mazalia ya viumbe hao, wale wanaopatikana huuzwa kwa bei ya juu, jumla na rejareja.

Samira Mohamed (26) mkazi wa Kunduchi anasema inawalazimu yeye na wenzake kuchanga Sh20,000 kila mmoja ili kununua ndoo ya samaki inayo gharimu Sh80,000.

“Samaki walipokuwa wakipatikana kwa wingi ilikuwa raha sana, tulikuwa tunanunua ndoo moja kwa Sh40,000 tu. Sasa hivi tunachanga wanne kununua ndoo ya Sh80,000 na faida unapata kidogo,” anasema Samira.

Uhaba wa samaki unawatesa hadi mama ntilie ambao ili angalau kupata faida kidogo baadhi yao humkata samaki katika vipande viwili badala ya kumweka mzima kama ilivyokuwa awali.

Mbali na kugawa vipande, baadhi ya vibanda vinavyouza chakula sasa vinauza samaki kwa bei ya juu ukilinganisha na nyama na vitoweo vingine na kuwafanya wasio na kipato kikubwa kutomudu.

Mamalishe na wauza chipsi wanaeleza kuwa samaki sasa wamekuwa kitoweo kisichokimbiliwa kirahisi na wateja kama awali. “Wateja wengi wakija huuliza samaki lakini nikiwaambia nauza Sh2,500 huulizia chakula kingine,” anasema Mama Tina anayeuza chakula Mtaa wa Mpakani, Mwenge jijini hapa.

Wengi waliofika katika mgahawa wa Mama Tina, uliokuwa umefurika wanafunzi, wafanyakazi na kinamama, waliagiza ugali nyama, wali nyama, ugali dagaa na ni wateja wawili tu kati ya waliokuwapo mgahawani hapo ndio waliokuwa wameagiza wali samaki.

Athari za mabomu

Chama cha Uhifadhi Wanyamapori Duniani (WCS) kinaeleza kuwa uvuvi wa mabomu unatishia soko la samaki nchini, utalii wa kuogolea na hatari kwa usalama wa Taifa.

Wataalamu wa viumbe wa baharini wanaeleza kuwa uhaba wa samaki unaoendelea kwa sasa hauhusiani na msimu wa hali ya hewa baharini bali matumizi ya mabomu yaliyokuwepo na kuathiri matumbawe ambayo ni muhimu kwa mazalia ya samaki.

Baada ya mabomu kupigwa, matumbawe huharibika na baadhi ya viumbe vya baharini ambao husalimika katika kadhia hiyo kama samaki hulikimbia eneo husika na kwenda mbali zaidi ambako si rahisi kwa mvuvi mwenye vifaa duni kuwavua.

“Viumbe vingi vya baharini hutegemea matumbawe kwa sababu wanapata chakula na hifadhi. Pia, ‘mangrove’ (miombo) ambayo ni chakula kwa samaki huharibiwa na mabomu yanayopigwa na wavuvi haramu,” anasema John Mchiwa, Profesa wa Sayansi ya Viumbe wa Majini na Uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Ili matumbawe yarudi katika hali yake ya kawaida na kuzalisha samaki kwa wingi, huchukua muda mrefu na kuacha wavuvi wakilia na ukame huku walaji wa samaki wakihaha kupata kitoweo hicho.

Ofisa katika Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi na Bahari wa Mfuko wa Wanyamapori Duniani (WWF), Lydia Mwakanema anasema tafiti zinaonyesha kuwa mwamba wa matumbawe, ambao samaki hupenda kuwepo kwa ajili ya chakula na mazalia, huchukua takriban miaka 100 ili kufikia urefu wa nchi moja.

“Sasa kitu ambacho kimekua miaka 100 kufikia ukubwa wa nchi moja hebu fikiria ukikiharibu madhara yake yanakuwa ni makubwa namna gani. Kwa hiyo kuyarudisha katika hali ya awali maeneo yaliyopigwa mabomu inachukua muda mrefu sana,” anasema Mwakanema na kuongeza: “Wakati mwingine ni kama haiwezekani na hasa kama maeneo ambayo ni miamba ya matumbawe.”

Watalii wapungua

Mmoja wa wavuvi wa Kigamboni ambaye hakutaka kutaja jina lake, anasema uvuvi wa mabomu umepunguza kasi ya watalii waliokua wakitembelea Kigamboni na kupiga mbizi ili kuangalia viumbe baharini.

“Zamani walikuwa wanakuja wengi hapa kuzamia kuangalia samaki chini ya bahari, lakini sasa mabomu yamewafukuza. Watalii wengi wamesitisha kuja si kama zamani,” anasema.

Mabomu yanayotumika kuvulia yameathiri hadi wavuvi wenyewe ikiwamo baadhi kufariki au kujeruhiwa viungo na kubaki na vilema. “Baadhi wamefariki dunia na wengine wamekatika mikono. Hata mimi kidole hiki hakikukatwa kwa panga ila ilitokea wakati wa kurusha bomu baharini bahati mbaya sikuona kama limewaka, sasa katika kujitetea likanikata kidole,” anasema Omary Mussa Omary, mvuvi wa Kimbiji jijini hapa ambaye alijisalimisha kwa mamlaka na kuachana na uvuvi huo.

Lindsey West, Mkurugenzi wa Sea Sense, taasisi inayojihusisha na uchunguzi wa samaki na viumbe bahari anaesema ni vigumu kuwapata watu waliopata madhara hayo kwani shughuli nyingi za aina hiyo hufanyika kwa siri.