Uwanja wa Kia wageuka mwiba kwa wauza unga

Abiria wakiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro baada ya kushuka kwenye ndege. Picha na Mtandao

Muktasari:

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baada ya agizo hilo vyombo vya ulinzi na usalama viliongeza umakini na hadi kufikia wiki iliyopita raia 10 wa kigeni na Watanzania wametiwa mbaroni.

Moshi. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) ambao ulikuwa ukisifika kuwa uchochoro wa usafirishaji dawa za kulevya, sasa unatajwa kuwa mwiba kwa wauza unga.

Novemba 2013 aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk Harrison Mwakyembe aliwaonya maofisa wa umma katika uwanja huo kuugeuza njia ya kupitishia dawa hizo.

Dk Mwakyembe alikaririwa akisema taarifa alizokuwa nazo zilionyesha baadhi ya Watanzania waliokamatwa nje ya nchi na hati bandia za kusafiria walipitia uwanjani hapo.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baada ya agizo hilo vyombo vya ulinzi na usalama viliongeza umakini na hadi kufikia wiki iliyopita raia 10 wa kigeni na Watanzania wametiwa mbaroni.

“Kwa mwenendo wa Serikali hii ya Rais Magufuli nani anataka kuharibikiwa? Kila section (idara) sasa wapo makini maana dawa zikipitia eneo lako ujue unalo,” alisema ofisa mmoja wa usalama wa Kia.

“Dk Mwakyembe alipokuja hapa alipiga mkwara sana kwamba mtu akikamatwa na dawa Serikali itafuatilia nani waliokuwa zamu siku hiyo. Unaona ni shwari hapo kweli?”

RPC K’njaro atoboa siri

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alipoulizwa siri ya mafanikio hayo, alisema vyombo vya ulinzi na usalama uwanjani hapo vinafanya kazi kama timu moja.

Kwa mujibu wa Kamanda Issah, udhibiti ni matokeo chanya ya ushirikiano wa kamati ya ulinzi na usalama katika uwanja huo uliosababisha mianya iliyokuwapo awali kubanwa.

“Kupambana na dawa za kulevya ni vita na utekelezaji wake unahitaji mikakati ya kidunia, unaohusu viwanja vya ndege na pale Kia sasa hivi kuna mashine za kisasa lazima tuwakamate,” alisema.

“Kamati ya ulinzi na usalama Kia inashirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha hakuna biashara haramu inayopita uwanjani hapa. Mizigo yote na abiria wanakaguliwa kikamilifu.”

Raia kigeni kufia gerezani

Tangu Dk Mwakyembe awashe moto katika uwanja huo, raia wa kigeni na Watanzania wapatao 10 waliojaribu kupitisha ‘unga’ wako magerezani.

Hukumu ya karibuni ilitolewa Machi 7, ambapo raia wa Liberia, Grace Gbatu alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kusafirisha gramu 10,064 za heroin. Grace alitiwa hatiani kwa kusafirisha dawa hizo zenye thamani ya Sh603 milioni kwenda Free Town, Siera Leone. Alikamatwa uwanjani hapo baada ya ukaguzi.

Februari 27, Josephine Mumbi Waithera, raia wa Kenya alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kusafirisha gramu 3,249 za heroin kupitia Kia.

Pia Februari 22 raia wa Uholanzi, Vania Diamers alihukumiwa kulipa faini ya Sh4 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 29.359 za mirungi kwenda nchini kwao. Mbali na hao, Aprili 10, 2018 mkazi wa Dar es Salaam, Rukia Mohamed alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kusafirisha gramu 1,471 kwenda Enugu, Nigeria.

Oktoba 10, mwaka huo raia wa Brazil, Joao Olivera alifikishwa kortini kwa tuhuma za kusafirisha gramu 5,800 za cocaine na hadi sasa yuko mahabusu akisubiri kesi yake kusikilizwa.

Hali kadhalika, Julai 16, 2018 raia wawili wa Marekani - mume na mke, Dorotea Sheikh na Imitiaz Shekh walifikishwa kortini kwa kusafirisha gramu 4,888 za heroin.

Raia wengine wa kigeni waliofungwa maisha ni yule wa Togo, Josian Dede (1,989) na Joachim Ikechukwu wa Nigeria (6,969). Hata hivyo Dede alikata rufaa na kesi yake inasikilizwa upya.

Miongoni mwa waliofungwa maisha wapo Watanzania na uzito wa dawa ukiwa kwenye mabano akiwamo Hamis Suya (3,191.3) na Salome Kingazi (3,379) ambaye pekee alifungwa miaka 20.

Habari ya nyongeza na Zainabu Maeda