VIDEO: Glory Mziray alivyoimaliza siku yake ya mwisho duniani

Muktasari:

Mwili wa Meneja Mawassiliano na Uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Glory Mziray aliyefariki dunia Jumanne wiki hii, unasirishwa leo kwenda Mikese mkoani Morogoro kwa maziko yatakayofanyika kesho. Glory amefariki kama mshumaa uliozimika ghafla kwani katika siku yake ya mwisho hapa duniani aliendelea na shughuli zake za kikazi na kijamii ikiwemo kupokea zawadi ya Valentine aliyoelea kupendezwa nayo.

Inaweza kuonekana ni kama filamu jinsi Meneja Mawasilino na Uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Glory Mziray alivyomaliza safari yake hapa duniani.

Glory alifikwa na umauti juzi mchana akiwa ofisini kwake katika jengo la Mpingo ambalo huko nyuma liliwahi kutumika kama makao makuu ya wizara ya maliasili na utalii pamoja na baadhi ya taasisi zake ikiwamo TFS.

Siku Glory alipokutwa na umauti, TFS ilikuwa na mkutano na waandishi wa habari na mzungumzaji mkuu alikuwa yeye ambapo alionekana akiwa amejiandaa vilivyo kutekeleza jukumu hilo.

Nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo na nilipowasili ukumbini nilimkuta Glory akiwa tayari ameketi kwa ajili ya kuanza kuzungumza.

Tukasalimiana na kuleta utani wa hapa na pale akionekana mwenye bashasha na afya njema wala usingeweza kutilia shaka uhakika wa yeye kuimaliza siku ile kutokana na tatizo la kiafya.

Punde akaanza kuzungumza kwa kusoma taarifa aliyoaindaa akiueleza umma juu ya kupandishwa hadhi kwa misitu saba iliyopo nchini.

Haikumchukua zaidi ya dakika 15 alimaliza kusoma maelezo yote na kushukuru kwa kusikilizwa.

Nikanyoosha mkono huku nikieleza kuwa nataka kuuliza maswali, lakini kabla hajaruhusu akatokea mwandishi mwingine wa televisheni akamtaka aseme jina lake na cheo chake kwa kuwa alianza kuzungumza bila ya kufanya hivyo.

Wakati anatamka jina lake na cheo chake ghafla sauti ilianza kubadilika na akaonekana kama mwenye shida fulani hivi.

Tulipomsogelea kumpa msaada alikuwa amepoteza fahamu, akatolewa nje kwa ajili ya kupata hewa huku wengine wakimpepea.

Ukaandaliwa usafiri kwa ajili ya kumpeleka hospitali, garini Glory alilazwa kiti cha nyuma na muda wote kichwa chake kililazwa kwenye mapaja yangu.

Safari kwenda hospitali ikaanza na palipoonekana kuwa jirani zaidi ni katika kituo cha afya cha TMJ kilichopo Chang’ombe.

Haikuchukua dakika 10 alifikishwa hospitali na kuingizwa kwenye chumba maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu. Baada ya kumfanyia uchunguzi madaktari wakaeleza kuwa Glory alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.

Mganga aliyempokea, Dk Chris Peterson alieleza kuwa kwa taarifa alizozipata kutoka familia ya marehemu kuhusu historia yake inaonyesha Glory alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.

Taratibu zilifanyika kuitaarifu familia yake ambayo ilifika kituoni hapo haraka na kufanya mchakato wa kuhamishia mwili wake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kabla ya kwenda kazini alianzia katika hospitali ya Masana ambako alifanyiwa ukaguzi wa afya yake na kuonekana hakuwa na tatizo kubwa linaloweza kumzuia kuendelea na shughuli zake.

Apokea zawadi ya Valentine

Rafiki wa Glory, Mariam Kobelo ambaye ni Ofisa Masoko wa TFS, anasema jana ndipo alipomkabidhi zawadi aliyokuwa amewandalia kwa ajili ya siku ya Wapendanao (valentine day).

Anasema ingawa aliiandaa tangu Februari 10, lakini walikuwa hawajapata muda wa kukutana na kwamba ni jana ndipo alipoipokea na kushukuru.

“Tulikuwa hatujapata muda wa kukutana, nilimtumia mtu kumfikishia naye akanijibu ameipata na kuifurahia,” alisema Maria.

Jinsi nilivyokutana na Glory

Kwa mara ya kwanza nilikutana na Glory Septemba mwaka jana, wakati wa maandalizi ya shindano la Miss Tanzania ambalo TFS walikuwa miongoni mwa wadhamini.

Katika udhamini huo TFS ilitoa fursa ya washiriki wa Miss Tanzania kwenda kutembelea msitu wa Amani ulioko mkoani Tanga kwa ajili ya kuangalia vivutio na kuvitangaza duniani.

Glory alikuwa kiongozi wa msafara huo kwa upande wa waandishi wa habari na hapo ndipo nilipopata nafasi ya kumfahamu.

Wakati wote wa safari alikuwa mcheshi na mwenye kujichanganya na waandishi akishiriki ‘kupiga stori’ (mazungumzo) na vichekesho vilivyokuwa vikitolewa ndani ya gari. Safari ikawa nzuri tulizunguka msitu huo, tukitembea na kupiga picha huku na kule sote tukifurahia mazingira hayo.

Bila wasiwasi Glory nae alikuwa huru kupiga picha na wakati mwingine aliomba umpige picha katika eneo ambalo aliona linamvutia.

Ziara ikaisha, safari ya kurejea Dar ikaanza, lakini kutokana na ubovu wa miundombinu kutoka Amani, tulipofika Muheza ilibidi gari letu lisimame kuwasubiri warembo ambao walipanda gari lingine na tuliwaacha kwa umbali mrefu. Nakumbuka ilikuwa saa moja jioni tulipofika Muheza, waandishi hasa wa video wakapata fursa ya kutuma habari, mimi na Glory tukatoka kwenda kutafuta maliwato kisha kula chakula cha jioni.

Ukaribu haukuishia pale kwani Glory alifurahishwa na namna waandishi wa habari walivyofanya kazi katika ziara hiyo na kuamua kuanzisha ‘group’ (kundi) kupitia mtandao wa WhatsApp akitekeleza wazo alilolitoa tangu tukiwa njiani tukirejea Dar kutoka Amani ambako utani, ucheshi ukaendelea kwenye kundi hilo.

Maziko yake

Kwa mujibu wa mjomba wake, Epharahim Kakwabanga, mwili wa Glory jana ulitarajiwa kulala nyumbani kwao, Kinzudi, Goba ambapo leo utasafirishwa kwenda Mikese, Morogoro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho.