VIDEO: Mradi wa Kilimanjaro unaohamasisha juhudi za kurejesha uoto asilia nchini

Muktasari:

Mradi huo umekuja na mikakati mbalimbali ya kuishirikisha jamii katika udhibiti na kulinda misitu nchini, huku ukiwa pia na lengo la kuhakikisha kuwa Mlima Kilimanjaro unatunzwa ili kutoathiri theluji kileleni

Kuna kanuni moja ya mwanasayansi Isaac Newton inasema kwa Kiingereza “for every action (force) in nature, there is an equal and opposite reaction”.

Yaani kwa kila kitendo (nguvu) asilia, kuna nguvu kinzani na iliyo sawa nayo. Au kila nguvu unayoweka kwenye kufanya jambo ndiyo nguvu unayoipata kutoka kwenye jambo hilo. Kanuni hii inaakisi kwa namna kubwa jinsi nguvu ya ukataji misitu nchini Tanzania ilivyosababisha athari nyingi za kimazingira.

Ukataji wa miti kwa ajili ya shughuli za kilimo na kupata nishati ndio umekua chanzo kikuu cha uharibifu mkubwa wa mazingira, na kusabababisha maeneo mengi kuwa jangwa na pia kuathiri hali ya hewa.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 85 ya nishati inayotumiwa na wananchi wote wa Tanzania ni kuni na mkaa. Na upatikanaji wa nishati hiyo husababisha eka 400,000 za miti kukatwa kila mwaka.

Kwa kuwa msukumo mkubwa wa ukataji miti hutokana na mahitaji ya wananchi, hivyo hata utatuzi wa athari zake unatakiwa utafutwe na wananchi wenyewe.

Ndivyo anavyoshauri Sarah Scott, mwanaharakati wa utunzaji mazingira na mwanzilishi wa programu ya upandaji miti (Kilimanjaro project).

Scott anasema kila Mtanzania anatakiwa awajibike katika kurudisha uoto wa asili nchini kwa njia ya kupanda miti kwa kuwa kwa namna moja ama nyingine amechangia ukataji wake.

“Si lazima ushike panga mwenyewe na kukata mti, lakini ile demand (hitaji) kubwa iliyopo kwenye bidhaa zinazotokana na misitu, imesababisha muendelezo wa uharibifu wa mazingira,” anasema Scott.

Anasema ni wajibu wa kila Mtanzania kupanda miti kwa sababu asilimia 90 ya watu wote hutegemea nishati itokanayo na miti.

“Shocking (inashangaza) kwamba ukipiga mahesabu eka 400,000 ni wastani wa viwanja vya mpira milioni moja na laki mbili,” anasema balozi wa mradi huo wa Kilimanjaro, Joe Legendary.

Legendary anasema nyumba moja hutumia wastani wa mti mmoja kila mwezi, hivyo ni miti kumi na mbili kwa kila nyumba kila mwaka.

“Watu hawajui tu. Hata huku kuongezeka kwa joto na ukosefu wa mvua ni matokeo ya ukataji wa miti. Kwahiyo tujue dependency (utegemezi) wetu kwenye nishati zinazotokana na misitu umeleta matatizo yote haya na ni lazima tuwajibike,” anasema.

Legendary anasisitiza kuwa uharibifu mkubwa wa mazingira umechangia pia maeneo yaliyokuwa na hali ya hewa ya baridi kama Kilimanjaro kuwa na joto kali.

“Kwa mtu ambaye hajasoma jiografia, si rahisi kuelewa moja kwa moja. Lakini ukweli ni kwamba misitu huchangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa mvua,” anasema balozi huyo.

“Mvua nayo ina umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku, kwa kutupatia maji safi na kukuza mazao shambani. Ukosefu wa mvua kwa muda mrefu husababisha ukame na baa la njaa.”

Kuhusu mradi

Mwaka 2018, Scott alianzisha mradi wa upandaji miti na kuuita The Kilimanjaro Project (Mradi wa Kilimanjaro) kwa lengo la kuongeza ufahamu wa jinsi gani uharibifu wa mazingira umechochea athari ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Kampeni hiyo hutumia ishara ya mlima Kilimanjaro kama kiashiria wazi cha athari hasi za mabadiliko ya hali ya hewa, baada ya wataalamu kuripoti jinsi barafu iliyopo kilele cha mlima huo inavyoyeyuka siku hadi siku.

“Ni mradi unaoelezea uharibifu wa mazingira na athari zake katika jamii. Kimsingi tunataka kupaza sauti duniani kote na tunatumia mlima Kilmanjaro kwa sababu unatambulika kimataifa,” anasema Scott.

Anasema kupitia mradi huo wanataka kujiunga na majadiliano ya kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na pia kuwakusanya watu pamoja ili kutafuta suluhisho endelevu ambalo ni pamoja na kupanda miti mingi kila mwaka.

Kwa mujibu wa Scott, mradi huo ulianza kama kampeni ya kuongeza ufahamu, lakini sasa upo katika hatua ya vitendo zaidi ikiwa ni pamoja na kupanda mamilioni ya miti katika mkoa wa Kilimanjaro na kote nchini.

Katika operesheni ya kwanza chini ya mradi huo mwaka jana walifanikiwa kupanda miti 75, 000 katika wilaya nne za mkoa huo.

“Tulipanda kwenye baadhi ya shule na maeneo ya ofisi za serikali ya mitaa, pia katika maeneo ya hifadhi za mito,” alisema Scott.

Balozi wa mradi huo, Legendary alisema lengo la awali lilikuwa ni kupanda miti 100,000.

“Kidogokidogo ndivyo tunavyoenda na tunathamini maendeleo mazuri ambayo mradi umefanya na tunategemea kupanda miti mingi zaidi mwaka huu”.

Hata hivyo, Scott anasema wakati muafaka wa kukabiliana na ukataji miti ni sasa na kwamba msukumo huo aliupata baada ya kufanya mahojiano na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

“Mheshimiwa alitoa wazo ambalo lilinipa msukumo mkubwa sana. Alisema hebu fikiria. Kama kila Mtanzania akipanda mti mmoja tu kila mwaka, tutakuwa tunapanda miti milioni hamsini kila mwaka,” anasema Scott.

Anasema Mradi wa Kilimanjaro ni ndoto yake ya kuhimiza kila Mtanzania kupanda angalau mti mmoja kila mwaka.

“Idadi ya watu inaongezeka kwa kiwango cha juu na hii  itakuwa na athari kwenye  mazingira. Kwa maana hiyo tunapopanda miti mingi zaidi ndipo tunapojihakikishia faida kwa vizazi vijavyo,” anasema.

‘Tuje Pamoja’ ni mojawapo ya kampeni iliyoanzishwa chini ya Mradi wa Kilimanjaro ili kuhamasisha watu kujitolea na kuunga mkono juhudi za kurejesha uoto wa asili.

Legendary alisema shirika pia limeanzisha programu ya kufuatilia miti ambayo itazinduliwa hivi karibuni. Programu hiyo itakuwa inaunganisha mradi pamoja na wadau wake, na pia itaweka uwazi wa matumizi ya fedha zilizochangwa na wafadhili.

Programu hiyo inaweza kupakuliwa kwa njia ya simu na hivyo kuwezesha watu kufuatilia maendeleo ya miti yao moja kwa moja kwa njia ya GeoTAG.

“Na tutaweka namna ambayo mtu anaweza kupata kiasi cha pesa kutoka katika programu hiyo,” alisema.

Scott alisema nguzo ya programu ya kufuatilia miti ni ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Green Stand.

“Kwa kweli kupanda ni rahisi, lakini kufuatilia maendeleo ni jambo jingine. Kusipokuwa kuna motisha ya kiuchumi kwa watu, miti haiwezi kudumu. Kwa hiyo programu hii itatuwezesha kufanya hivyo,” alisema.

Mradi wa Kilimanjaro pia unahusisha ushirikiano na wasanii kama Vanessa Mdee na Idris Sultan, pamoja na wadau wengine wa mazingira.

Scott anasema pia wanapata ushirikiano kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba pamoja na marais wastaafu; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Nishati Mbadala

Scott anasema ikiwa kuna uwezekano wa kaya kutumia aina nyingine ya nishati, wanapaswa kufanya hivyo ili kupunguza matumizi ya mkaa na ukataji miti.

“Kuna nishati mbadala kwa mkaa kama gesi ambayo inapatikana zaidi katika miji,  nishati ya ‘bayogesi’ na pia mkaa mbadala.”