VIDEO: Maswali sita ya Majaliwa kuhusu ajali ya moto iliyoua 69 Morogoro

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameuliza maswali sita kuhusu ajali ya moto iliyoua Watanzania 69 mkoani Morogoro huku akitangaza kuunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa ajali hiyo

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameuliza maswali sita kuhusu ajali ya moto iliyoua Watanzania 69 mkoani Morogoro huku akitangaza kuunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi Agosti 10, 2019 katika kijiji cha Itigi, Msamvu mkoani Morogoro   baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uwanja wa shule ya sekondari Morogoro kwa ajili ya kuaga miili ya waliokufa katika ajali hiyo, Majaliwa ameitaka kamati hiyo kutoa majibu Ijumaa Agosti 16, 2019.

Picha za video zinaonyesha lori hilo likiwa limepinduka barabarani na mafuta yakichuruzika kuelekea pembeni mwa barabara ya Morogoro- Dar es Salaam ambako watu waliokuwa na madumu ya ujazo mbalimbali walikuwa wakichota mafuta kabla ya moto kuwaka.

Akizungumza kwa mtindo wa kuuliza maswali, Majaliwa alianza na swali la kwanza na kusema, “Ajali ilipotokea kila mmoja kwa majukumu yake aliwajibika?”

Katika swali la pili amesema, “Ajali ilipotokea ni mahali palipo na shughuli nyingi za kijamii ikiwemo kituo kikuu cha mabasi tuna trafiki hapo, tuna polisi wa ulinzi hapo. Ilipoanguka tu nani alitokea wa kwanza.”

“Na hawa ndugu zetu waliotangulia mbele za haki ni wale ambao walikuja na madumu kuja kuchota mafuta. Unataka kuniambia hao watu walijua lori litaanguka leo litaanguka wakaja asubuhi? Au walipata taarifa au wengine walipoona limeanguka wakakimbia nyumbani kuchukua madumu. Je huu muda wa kukutana hawa watu wote tuliowapoteza ni nani aliwajibika kuwazuia,” amesema Majaliwa katika swali lake la tatu.

Katika swali lake la nne amehoji kama askari wa kikosi cha usalama barabarani walichukua hata uamuzi wa kukodi gari kuwahi eneo la tukio baada ya kupata taarifa.

“Tumeweza kuona watu wamekuja pale (kuchota mafuta) kabla ya yule aliyekuja kuchomoa betri (moto kuibuka), wengine walichota na kuondoka, nani alihusika kuwazuia,” amesema Majaliwa.

Katika swali la sita, Majaliwa alizungumzia Manispaa ya Morogoro kuwa kitengo cha kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, “Najua walikuja baadaye kuzima, naamini taarifa zilisambaa kuhusu tukio hilo je walikuja baada ya muda gani?”

“Kwa haya lazima tujiridhishe humu ndani ya Serikali kama kila mmoja aliwajibika.”

Waziri Mkuu ametaka Watanzania kutotumia ajali kama fursa bali kuokoa binadamu waliopo katika chombo kilichopata ajali.