VIDEO: Msekwa alivyowajibu Kinana na Makamba

Muktasari:

Ni kutokana na barua yao ya malalamiko

Dar es Salaam. Katibu wa baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa CCM, Pius Msekwa amewajibu kwa kuwaandikia barua makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Msekwa amewaandikia barua vigogo hao akijibu malalamiko yao waliyoyawasilisha kwake wakidai kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa serikali jambo ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama hicho na nchi.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, Jumapili iliyopita walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Tangu malalamiko hayo yalipotolewa, hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliye madarakani amejitokeza kuyazungumzia na Mwananchi limekuwa likiwatafuta mara kadhaa bila mafanikio.

Hata hivyo, Msekwa amewajibu vigogo hao katika barua aliyoiandika siku moja baada ya kupokea malalamiko hayo Jumatatu ya Julai 15 yenye kichwa cha habari: ‘Barua ya majibu ya awali’ kwa Kinana na Makamba.

“Kama mnavyofahamu, baraza hili hufanya kazi kwa njia ya vikao rasmi na kwamba katibu peke yake hana mamlaka ya kutoa maamuzi yoyote. Kwa hiyo, nitawasilisha barua yenu kwa wajumbe wa baraza ili kupata maelekezo yao juu ya nini kifanyike,” amesema spika huyo wa zamani aliyeongoza Bunge kati ya mwaka 1994 hadi 2005.