VIDEO: Profesa Kabudi ampa maagizo Makonda

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza katika mkutano wake na wamiliki na wakuu wa vyombo vya habari nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametakiwa na Waziri wa Mambo ya  Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba Kabudi kuzitafuta na  kuzitambua nyumba na ofisi zote zilizotumiwa na wapigania uhuru katika nchi mbalimbali za Afrika zilizopo Tanzania.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya  Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba Kabudi amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzitafuta na kuzitambua nyumba na ofisi zote zilizotumiwa na wapigania uhuru katika nchi mbalimbali za Afrika zilizopo nchini Tanzania.

Profesa Kabudi ametoa agizo hilo leo Jumatano Juni 12, 2019 wakati akizungumza na wamiliki na wakuu wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Amebainisha kuwa Agosti 17, 2019  Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) , ugeni aliodai pamoja na mambo mengine utafanya kumbukizi ya Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania.

“Wakuu wa nchi 16 watahudhuria mkutano huu na kuleta  ombi maalumu kufanya kumbukizi ya Nyerere watakapokuwa. Hii ni fursa kwetu kuweka kumbukumbu na ku identify (kutambua) maneno yote ambao wapigania uhuru wa nchi mbalimbali walikaa.”

“Tupitie nyumba zote walizokaa mfano Jacob Zuma (rais mstaafu wa Afrika Kusini) aliishi hapa,  Sam Nujoma (Rais mstaafu wa Namibia) na wengine wengi tuzitambue hizo nyumba na ofisi zao,” amesema Profesa Kabudi.

Waziri huyo amesema Watanzania wanaona kawaida uwepo wa nyumba hizo lakini ukweli ni kuwa zitasaidia kuweka kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.