VIDEO: Spika Ndugai asimamisha ubunge wa Stephen Masele Afrika

Spika wa Bunge, Job Ndugai akitangaza kumsimamisha Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Steven Masele kuwa mjumbe wa Bunge la Afrika (PAP) kutokana na utovu wa nidhamu ambapo amemtaka kurejea nchini kutoka Afrika Kusini, alipokuwa akisoma taarifa bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM) Stephen Masele ameingia katika mgogoro na Spika Job Ndugai pamoja na bunge la PAP akitajwa kuwa mtovu wa nidhamu.

Dodoma. Spika wa bunge Job Ndugai amemsimamisha kwa muda uwakilishi wa mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele katika bunge la Afrika (PAP) hadi taarifa rasmi zitakapotolewa.

Kutokana na hilo, amemtaka mbunge huyo kurudi haraka nchini ambako pia atafikia mikononi mwa kamati za maadili za Bunge na chama chake (CCM).

Katika taarifa yake bungeni leo Alhamisi Mei 16,2019, Spika wa bunge Job Ndugai amesema mbunge huyo amekuwa akifanya mambo ya hovyo na kugonganisha mihimili.

"Amefanya mambo ya utovu wa nidhamu huko  na taarifa tumezipata na hata kwenye mitandao imeonekana, sasa tumemtaka arudi lakini amegoma hivyo nimemwandikia barua Raid wa PAP kusimamisha kwa muda ubunge wa mheshimiwa huyu had I tutakapotoa taarifa nyingine," amesema Ndugai.

Akizungumzia kugoma kurudi kwa mbunge huyo, anasema alimtaka arudi toka jana lakini bado aliendelea kumgomea akisema Spika hawezi kumuita kwa kuwa ana kibali cha Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Ndugai, hata hapa nchini Tanzania mbunge huyo amekuwa na tabia zisizokuwa za kibunge ambazo zinalifanya bunge lisitambue msimamo wake ni upi.