Vanessa Mdee akwepa kumzungumzia Jux

Muktasari:

  • Msanii Vanessa Mdee  jana Jumamosi Julai 27, 2019  alifanya sherehe ndogo ya kukutana na watu wake wa karibu lakini kati ya mambo ambayo hakutaka kuyazungumza ni kuhusu mpenzi wake wa zamani, Jux.

Dar es Salaam. Msanii Vanessa Mdee  jana Jumamosi Julai 27, 2019  alifanya sherehe ndogo ya kukutana na watu wake wa karibu lakini kati ya mambo ambayo hakutaka kuyazungumza ni kuhusu mpenzi wake wa zamani, Jux.

Pamoja mambo mbalimbali alitambulisha albamu yake yenye nyimbo sita, baadhi akiwa ameimba na wasanii Rayvanny na Mboso.

Katika sherehe hizo zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu wasiozidi 50 wakiwemo wasanii maarufu, nyimbo hizo zilipigwa na kuonekana kuwakuna vilivyo.

Baada ya kuingia ukumbini, Vanessa alisalimiana na kila aliyehudhuria, baadaye kuitwa jukwaani na mshereheshaji, Perfect Crispin na kuanza kutumbuiza.

Moja kati ya nyimbo alizoimba ni wimbo Moyo unaotesa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.

Mwananchi lilipotaka kufahamu kuhusu sababu za kuvunjika kwa uhusiano wake na Jux, msanii huyo aligoma akitaka kuulizwa mambo yanayohusu sherehe hiyo.

Jux na Vanessa inaelezwa kuwa mahusiano yao yalivunjika miezi nane iliyopita, siri iliyotobolewa  na Vanessa mwenyewe baada ya kurusha kipande cha video akizungumzia suala hilo na kukiweka katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Hivi karibuni Jux ameonekana katika mitandao mbalimbali ya kijamii akiwa na mwanamke mwingine wakila raha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

“Hapa nimekuja kukutana na watu wangu wa karibu na kuwaonjesha albamu  yangu, sijaja  kumzungumzia Jux naomba uulize swali jingine,” amesema Vanessa.

Baadhi ya wasanii waliohudhuria sherehe hizo ni Shilole, Navy Kenzo, Mimi Mars na Whoze.