Vibarua vitano kwa Rais Ramaphosa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kula kiapo cha kuongoza Taifa la Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa atakabiliwa na vibarua vitano katika Ikulu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Shirika la Habari la AFP, jambo la kwanza ni kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi hiyo yenye miundombinu lakini ambayo imekuwa ikiathiriwa na utegemezi wa bidhaa kwa zaidi ya muongo. Tatizo la ajira linakaribia asilimia 27 huku wakazi milioni 20.3 sawa na asilimia 55.2 nchini humo wakiwa ni vijana wa umri kati ya miaka 15-34.

Jambo la pili ni changamoto ya usawa miongoni mwa wananchi wapatao milioni 56.7. Afrika Kusini inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye tabaka kubwa kati maskini na tajiri duniani. Tangu ilipomaliza vita ya ubaguzi wa rangi miaka 25 iliyopita, bado ubaguzi huo unawaathiri Waafrika katika ajira.

Kwa mujibu wa taasisi ya Race Relations nchini humo, asilimia 20 ya Waafrika wanaishi maisha duni ikilinganishwa na asilimia 2.9 ya Wazungu.

Jambo la tatu ni vita dhidi ya rushwa iliyosababisha kashfa ya Rais Jacob Zuma kuondoka maradakani mwaka jana kutokana na msimamo wa chama chake cha ANC.

Februari mwaka huu, Ramaphosa aliweka wazi nia yake ya kuanzisha kitengo cha majaji waandamizi saba kwa ajili ya kuongeza kasi ya usikilizaji wa kesi za rushwa kwa haraka.

Jambo la nne litakuwa ni kupambana na uhalifu ambao kwa mwaka jana umesababisha watu 19,000 kuuawa, sawa na 52 kwa siku kwa mujibu wa takwimu za mamlaka husika za nchi hiyo. Takribani wanawake 100 wameripotiwa kubakwa kila siku na ukatili wa kijinsia umeathiri taswira ya nchi hiyo duniani

Jambo la tano ni matarajio makubwa ya wananchi katika mabadiliko ya umiliki wa ardhi ambayo yataweka usawa kati ya raia wenye asili ya Afrika na kizungu. Sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo inadaiwa kuwa chini ya wananchi wenye asili ya kizungu.

“Hatua ya mabadiliko katika umiliki wa ardhi ni jambo tusiloliogopa hata kidogo, litakwenda kufanyika kikatiba,” Ramaphosa aliwaambia wakulima wa nchi hiyo Aprili mwaka huu.

“Ramaphosa anatakiwa kuhakikisha anafanyia uamuzi kwa makini sana katika suala hilo,” alisema Daniel Silke, mchambuzi wa siasa alipokaririwa AFP.