VIDEO: Vifo vyaendelea kuongezeka majeruhi wa ajali ya lori lililowaka moto Morogoro

Muktasari:

Majeruhi wengi wanahitaji kuongezewa dawa, Muhimbili yaomba msaada watu waendelee kujitokeza kuchangia damu ili kukidhi mahitaji

Dar es Salaam. Majeruhi 6 kati ya 38 wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefariki dunia na kufanya idadi ya waliofariki hadi sasa kufikia 82

Majeruhi hao ni wa ajali ya moto iliyotokea Morogoro baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka Moto.

Akitoa taarifa hiyo leo Agosti 14, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (MNH), Aminiel Aligaesha amesema kwa sasa wamebaki majeruhi 32.

Kati ya majeruhi hao 17 wapo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) huku wengine 15 wakiendelea kupatiwa matibabu katika wodi ya Sewahaji.

Mkuu huyo wa mawasiliano amesisitiza watu kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa kuwa bado kuna uhitaji mkubwa.

“Wapo wanakuja na kutuletea vijana wa kuchangia damu, niwashukuru kwa hilo na niwasisitize wengine waendelee kuja, damu inahitajika sana,”amesema Aminiel

Akizungumza katika eneo la kuchangia damu msanii Ahmed Olotu maarufu kama Mzee Chilo amesema ameguswa na tukio hilo na ndiyo sababu iliyomfanya kuhamasisha vijana kuchangia damu.

“Nimepatwa na uchungu mno lakini kwa kuwa umri wangu hauruhusu kuchangia damu, nimeona niwahamasishe vijana ninaofanya nao kazi waje kujitolea damu tuokoe maisha ya wengine,” amesema Mzee Chilo