Vifo wanaojifungua kwa upasuaji balaa

Daktari bingwa wa maradhi ya wanawake na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Nathanael Mtinangi alisema licha ya utafiti huo, Tanzania ina vifo vichache vitokeavyo wakati na baada ya upasuaji.

Muktasari:

  • Watafiti wengine wamesema katika mataifa mengi Afrika, kuna tatizo la uhaba wa damu salama kwa ajili ya kuwaongezea wajawazito. Ripoti hiyo inashauri kuwe na damu ya kutosha na kuongeza wataalamu wa dawa za usingizi ili kupunguza vifo hivyo.

Dar es Salaam. Kiwango cha vifo vya wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji maarufu barani Afrika ni mara 50 ya nchi tajiri, utafiti mpya umeonyesha.

Kati ya wanawake 200, mmoja hufariki dunia wakati au baada ya upasuaji, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa wazazi 3,700 katika nchi 22 Afrika, kwa mujibu wa ripoti ya The Lancet Global Health.

Kwa kulinganisha na Uingereza, kati ya wanawake 10,000 wanaojifungua, mmoja hufariki dunia kutokana na upasuaji.

“Matokeo hayo yanaonyesha haja ya dharura ya kutatua na kuboresha upasuaji salama,” alisema kiongozi wa utafiti huo, Profesa Bruce Biccard katika tipoti hiyo.

Utafiti huo umeeleza kuwa vifo vingi vinavyoweza kuzuilika vinatokana na mfuko wa uzazi kupasuka kwa mama ambaye awali alikuwa na matatizo, kutokwa damu nyingi kabla ya kufanyiwa upasuaji au baada na matatizo yatokanayo na upungufu wa wataalamu wa usingizi.

“Uboreshaji wa upasuaji salama utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga,” alisema Profesa Biccard.

Watafiti wengine wamesema katika mataifa mengi Afrika, kuna tatizo la uhaba wa damu salama kwa ajili ya kuwaongezea wajawazito. Ripoti hiyo inashauri kuwe na damu ya kutosha na kuongeza wataalamu wa dawa za usingizi ili kupunguza vifo hivyo.

Matokeo haya ni sehemu ya utafiti wa matokeo ya upasuaji barani Afrika, ambao umefuatilia wagonjwa wote ambao walifanyiwa upasuaji katika hospitali 183 za nchi 22 kwa siku saba.

Upasuaji wa kujifungua umeonekana kuchukua nafasi kubwa katika huduma zote za upasuaji wakati wa utafiti huo.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa asilimia 75 ya kesi zilizochunguzwa, ilikuwa ni wajawazito waliofikishwa vyumba vya upasuaji wakiwa na hali mbaya.

Kwa sasa, inaonyesha idadi ya wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji imeongezeka duniani kote ikiwa ni mara mbili zaidi. Nchi kama za Brazil, Misri na Uturuki nusu ya wajawazito hujifungua kwa upasuaji.

Akizungumzia utafiti huo, Daktari bingwa wa maradhi ya wanawake na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Nathanael Mtinangi alisema licha ya utafiti huo, Tanzania ina vifo vichache vitokeavyo wakati na baada ya upasuaji.

“Japokuwa sina takwimu, wajawazito wanaofariki baada ya kufanyiwa upasuaji, ni wachache zaidi kuliko wanaojifungua kwa njia ya kawaida,” alisema.

Alizitaja sababu zinazochangia vifo hivyo kuwa ni kutokwa damu nyingi, kifafa cha mimba, upungufu wa damu na maambukizi.