Vigogo wakiwamo Mbowe, Seth kupishana Kisutu kesho

Muktasari:

Kesho Alhamisi, kesi kubwa tatu zinazowahusu vigogo akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mfanyabiashara James Rugemalira watafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kusikiliza kesi zao.


Dar es Salaam. Vigogo wa kesi tatu tofauti akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe wanatarajia kupishana Mahakama ya Hakimu Makazi Kisutu jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi Januari 31, 2019 kusikiliza kesi zao.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walikula sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiwa gerezani baada ya kufutiwa dhamana.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana zao Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 112/ 2018 ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Wengine ni Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai. Kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari Mosi na FebruarI  16,  2018  maeneo ya  Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili wafanyabiashara wawili maarufu nchini, Habinder Seth na James Rugemarila, inatarajia kutajwa pia katika mahakama hiyo.

Seth na Rugemalira wanaendelea kusota rumande, takriban mwaka moja na miezi saba sasa, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, hata hivyo kesi yao inatarajia kutajwa kesho.

Wakati huo huo, kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh10.8 milioni inayowakabili, mawakala 10 wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL), itatajwa mahakamani hapo.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh10.8 milioni kwa lengo kuwakatia watu tiketi za ndege za shirika hilo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Fabian Ishengoma, Adam Kamara, Marlon Masubo, Alexander Malongo, Tunu Kiluvya, Jobu Mkumbwa, Mohamed Issa, Godfrey Mgomela, Absalom Nyusi na Janeth Lubega.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 10 na Oktoba 9, 2018, katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.