Vijana wapewa somo la kutunza misitu, kupanda miti

Monday April 15 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Mrembo wa Tanzania namba mbili, Nelly Kazikazi amewataka vijana kushiriki kikamilifu katika kutunza misitu iliyopo nchini huku akisisitiza kuna kila sababu ya kuwa na utaratibu kwa kila mmoja wetu kupanda miti.

Mrembo huyo ambaye pia ni balozi wa misitu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) amesema vijana wanapaswa kutambua thamani ya misitu nchini na kuhakikisha wanashiriki kuilinda na kwamba wasidharau misitu kwani faifa zake nyingi na hivyo ni vema wakahamasika kuingeza badala ya kuipunguza.

Kazikazi ameyasema hayo jana Jumapili Aprili 14,2019 aliposhiriki kupanda miti katika msitu wa Pugu akiwa na baadhi ya wanafunzi wa shule ya kimataifa ya Tanganyika (IST).

 “Nawahamasisha vijana wenzangu tuongeze namba ya misitu, tuwe na uaminifu kwa kupanda miti kadri tunavyoweza. Nafahamu wapo wanaokata miti kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kibadamu lakini ni vema sote kwa umoja wetu tukapanda miti.”

"Tunahitaji hewa safi ambayo inatokana na miti. Tunahitaji kivuli na kubwa zaidi misitu ule ukijani wake unaleta faraja kwa maisha ya binadamu," amesema Kazikazi ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Ashton Media Tanzania inayojihusisha na utengezaji wa mabango ya matangazo, Abbas Hirji amesema kampuni yao imeamua kushirikiana na TFS kutoa elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji misitu na kufafanua kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira.

"Ukiwa chini huwezi kuona uharibifu ambao umefanyika katika misitu yetu lakini ukiwa kwenye ndege utaona namna ambavyo moshi unaotokana na watu wanaokata miti na kuchoma mkaa. Misitu yetu inaharibiwa sana tumeona ipo haja ya kushiriki katika hili ili kusaidia vizazi vijavyo.”

"Kufanikisha hilo tumetengeneza mabango ambayo yanazungumzia utunzaji wa misitu kupitia jumbe mbalimbali, tunaamini kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia kutoa elimu ya kutunza misitu yetu," amesema Hirji .

Ofisa Misitu Mkuu Ugavi na Uenezi kutoka TFS, Shaban Kihula amesema taasisi hiyo imejipanga kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha misitu inatunzwa na ile ambayo imeharibiwa basi inarejeshwa kwenye uasili wake.

Amesema katika kuhakikisha malengo hayo wanafanikiwa wameamua kushirikiana kwa karibu pia na wanafunzi wa shule mbalimbali na vyuo kwa kuamini kwamba kwa kufanya hivyo idadi ya mabalozi wa misitu itaongezeka na kuondoa tatizo la uharibifu.

Advertisement