Viongozi wa dini Tanzania wataka kodi itumike kugharamia bima ya afya kwa kaya masikini

Thursday August 15 2019

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Kamati ya dini mbalimbali kuhusu uchumi na haki za jamii, imeishauri Serikali ya Tanzania kutumia sehemu ya kodi kugharamia gharama za matibabu kwa kaya milioni tatu nchini humo ambao utafiti umeonesha hawana uwezo kabisa wa kujigharamia huduma hizo.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ,Dk Steven Munga amesema hayo jana Jumatano Agosti 14,2019 katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa madhehebu ya dini yanayotoa huduma za afya katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Askofu Munga ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema utafiti uliofanywa na kamati hiyo umebaini ili kufanikiwa katika maendeleo ni muhimu kila mwananchi kuwa na afya njema ambayo inatokana na bima ya afya.

“Tumeona kuna kaya maskini sana ambao hawawezi kabisa kuchangia gharama ya bima ya afya na kutoa fedha taslimu wanapougua.”

“Hivyo tunapendekeza uwepo utaratibu wa kuwachangia kwa njia ya kodi ili kuyawezesha haya makundi mengine kuguswa na huduma hii muhimu kwa sababu afya ni jambo la msingi sana,” alisema Askofu Munga

Alisema mpango wa bima ya afya unapaswa kuwa shirikishi kwa kuwafikia walengwa na kutoa fursa ya mjadala mpana ili kuhakikisha huduma za afya ya jamii inamfikia kila mwananchi hata ambaye hana uwezo wa kuigharamia.

Advertisement

Kaimu Sheikh wa mkoa wa Kilimanjaro, Shaban Mlewa alisema wakiwa viongozi wa madhehebu ya dini wametembelea katika hospitali mbalimbali kujifunza na kuona utaratibu wa bima ya afya namna ulivyo na  manufaa makubwa .

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Sera kutoka Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Gloria Mafole alisema Serikali ya Tanzania imeridhia tamko la Abuja la kutenga asilimia 15 ya bajeti ya mwaka kuelekezwa katika sekta ya afya lakini Serikali imekua ikitenga asilimia 10 pekee na kusababisha mzigo kuwa mkubwa kwa wananchi wake.

 

Imeandikwa na Filbert Rweyemamu, Zainabu Hassan na Elizabeth Elias

Advertisement