Viongozi wa dini wajitokeza kwa wingi mapokezi ya ndege

Viongozi wa dini wakiwa kwenye hafla ya mapokezi ya Ndege

Muktasari:

Sherehe za mapokezi ya ndege aina ya Airbus A220-300 zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ambao wamesoma dua kumwombea Rais John Magufuli kwa kuwezesha ndege hizo kupatikana.


Dar es Salaam. Viongozi wa dini wamejitokeza kwa wingi katika hafla ya kuipokea ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 katika  Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ambayo imewasili leo Ijumaa Januari 11, 2019.

Baadhi ya viongozi hao ni Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, mwakilishi wa makanisa ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania CPCT, Askofu Mwakibolwa; mwakilishi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania  (CCT), Padri Richard Kamenya; mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Paschal Kamugisha na Askofu wa Kanisa la FGBF, Zachary Kakobe.

Wengine ni Mchungaji Antony Lusekelo wa Kanisa la Maombezi, kiongozi wa Waadventist wa Sabato, Askofu Steven Ngusa, kiongozi wa Kanisa la Agape, Venon Fernandes na Askofu Silvester Gamanywa.

Mbali na viongozi wa dini, hafla hiyo imehudhuriwa pia na mamia ya wananchi pamoja na viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za umma na vyombo vya ulinzi na usalama.

Rais John Magufuli anaongoza mapokezi ya ndege hiyo iliyopewa jina la Ngorongoro ikiwa ni karibu wiki tatu tangu alipopokea ndege ya kwanza ya aina hiyo, Desemba 23, 2018.

Ndege hiyo itafanya idadi ya ndege ambazo zimenunuliwa na Serikali na kuletwa nchini kufikia sita kati ya saba ambazo tayari zimenunuliwa.