Vita ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi yahamia mtandaoni

Muktasari:

Picha na taarifa za wakurugenzi zaidi ya 75 zawekwa mtandaoni wakitajwa kuwa makada wa CCM ili kuonyesha jinsi wengi wao ndiyo watakuwa wasimamizi wa uchaguzi

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku tatu tangu Serikali itangaze azimio la kupinga hukumu ya kuwaondoa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi nchini, baadhi ya watuamiaji wa mitandao wameanzisha kampeni ya kuipinga hatua hiyo.

Kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook, Twitter na Instagram, baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakitajwa kuwa makada wa CCM huku wakieleza kuwa kwa utaratibu huo hakuwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Katika mitandao hiyo kampeni hiyo inaendeshwa za hashtag ya Chaguzihuru, pumziyaCCM na WaTzsiwajinga zikiambatanishwa na picha mbalimbali za wanaodaiwa kuwa wakurugenzi wakiwa wamevalia sare za CCM.

Picha hizo zimeambatanishwa na majina ya wahusika, historia yao ya kisiasa na halmashauri anayoiongoza huku mwishoni zikiambatanishwa hashtag hizo tatu.

Mwanaharakati, Mariah Sarungi kupitia mtandao wa Twitter amesema Mahakama imeeleza wazi kuwa Katiba inakataza wasimamizi wa uchaguzi kuwa na ukada wa chama chochote.

Mtumiaji wa mtandao wa Twitter, Advoctae Katela alihoji walimu kutoruhusiwa kujihusisha na siasa wakati mwajiri wake ambaye ni mkurugenzi anasimamia uchaguzi.

Aliongeza kuwa suluhu ni kuzifanya nafasi za ukurugenzi ziingie katika mfumo wa ajira na siyo za uteuzi.

Shani Omar aliandika: Kitendo cha Serikali kukatia rufaa hukumu yenye tija kwa walio wengi kunadhihirisha ya kwamba ipo kwa maslahi ya kundi la watu fulani na siyo kwa wailo wengi.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa, Ngemela Lubinga amesema, "Mimi ninachofahamu hao wakurugenzi ni watumishi wa Serikali, sasa hayo mengine ni uchonganishi tu, ni majungu hayo, lakini ningependa uwasiliane na ofisi ya waziri Mkuu ndio wanaweza kujibu kwamba iliteua makada au watumishi wa serikali.”