Vitambulisho kaa la moto kwa Ma-RC

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameendelea kusisitiza suala la ugawaji vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ‘machinga’ kuwa litaondoka na kiongozi yeyote wakiwamo wakuu wa wilaya na mikoa watakaobainika kushindwa kutekeleza mpango huo.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mbinga mkoani Ruvuma ikiwa ni muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilomita 67 na thamani ya Sh134.712bilioni.

Hiyo ni mara ya pili kwa kiongozi huyo wa juu nchini kuzungumzia jambo hilo ndani ya siku saba baada ya Aprili Mosi kusisitiza kuhusu jambo hilo.

“Hivi karibuni nilitoa vitambulisho karibu milioni mbili, niliwapa wakuu wa mikoa na wilaya. Niliwaambia hivi vitambulisho mtakavyokuwa mkigawa mtakuwa mnawapa ulinzi vijana wetu waliokuwa wakinyanyaswa na kufukuzwa kila maeneo,” alisema Rais siku hiyo.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaapisha naibu katibu mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Sera, Adolf Ndunguru na naibu kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbipo.

“Hadi leo (Aprili Mosi ) sijapata ripoti yoyote inayoonyesha mkoa au wilaya iliyomaliza kugawa vitambulisho vyake na zimekusanywa kiasi gani cha fedha na kupelekwa TRA. Ungekuwa umeshaniletea ningeshajua ni mkuu wa mkoa gani hataki kufuata maagizo nimtoe au wilaya gani imekaa navyo,”alisema Rais Magufuli akiwaagiza viongozi wa TRA.

Jana alirudia kauli yake akiwa mjini Mbinga, “mimi ndiye niliyewachagua, nitaangalia nani amevigawa vitambulisho na vikaisha na kiasi cha fedha kilichoingia na nitaangalia watu gani wanasumbuliwa katika eneo lake.”

“Hili nitalifanya, atakayeshindwa kutekeleza maana yake hatekelezi ninayoyataka kuyatekeleza kwa wananchi wadogo. Msinilaumu na nyinyi wananchi chukueni hivi vitambulisho ili mgambo wakija muwaonyeshe, hawatawasumbua,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka wafanyabiashara wadogo kuwa na ujasiri kwa sababu wamekuwa wakinyanyaswa, ndiyo maana aliamua kutoa vitambulisho hivyo kuondokana na adha hiyo hasa katika kipindi chake cha urais.

“Najua itafika wakati wale wasiokuwa navyo mtasumbuliwa katika maeneo yenu ya biashara. Sitawatetea mkifukuzwa, kwa sababu mmeyataka wenyewe kwa kutochukua vitambulisho ambavyo ni ulinzi kwenu,” alisema

Aliwasisitizia wakuu wa wilaya na mkoa kutoa vitambulisho hiyo kwa wajasiriamali, lakini baadhi yao hawavitoi na kuna wengine wanaviuza kwa bei ya juu zaidi na kuvigawa kwa ulazima.

“Nimelisema tena hili, mheshimiwa Zambi (Godfrey-kaimu mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Lindi), kawaeleze wakuu wa mikoa wenzako hata message (ujumbe). Huwezi kuwa na viongozi unawaeleza kila siku, halafu hawatekelezi.”

“Maana yake wachague kufanya kazi au waondoke. Lazima watu wajue hizi kazi walizipenda, lakini ni za utumishi na za muda na ninapata shida, kweli urais mgumu… tena kweli hupati muda wa kumpuzika,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mawaziri wa awamu ya tano wana shida na kupata nafasi katika utawala wake ni mateso kwa sababu huna uhakika kama utamaliza nafasi yako bila kuondolewa, tofauti na miaka iliyopita.

“Enzi zetu ukiteuliwa uwaziri unajua hakika hata mwaka unamaliza, lakini hawa wana wasiwasi pia. Waombeeni pia wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala kwa sababu kazi hizi ni ngumu, hujui kesho itakuwaje,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa mkoa huo na kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha wanafuatilia na kuwabaini watu waliosababisha Benki ya Mbinga Community kufilisika na kusababisha kero kwa wakulima wa wilaya hasa wa kahawa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda kusema kumekuwa na changamoto mbalimbali katika vyama vya msingi hasa kwa wakulima waliopeleka kahawa nyingi kulipwa fedha kidogo lakini wanaopeleka kidogo kulipwa fedha nyingi.

“Nafahamu miaka ya nyuma kulikuwa na benki hapa, lakini naambiwa walioimaliza ni watu wa hapa. Muda mwingine matatizo ya kumaliza hapa tunasubiri hadi kiongozi mkubwa aje,” alisema Rais Magufuli

“Nimezungumza haya ili tutafute mzizi wa fitina, tukufunika funika hatutafika kwa sababu kuna watu wamefanya mambo ya ajabu huku wakitembea vifua mbele kwa utajiri wa mali za masikini waliowazudhulumu,” alisema.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema alitegemea Mapunda angemkabidhi orodha ya watu waliokuwa wanahusika na kununua kahawa na kuwadhulumu wananchi kuwa ni fulani na fulani badala yake anaficha na kuyafumbia jambo linaloashiria maana yake hataka kutafuta dawa ya changamoto hiyo.

“Nataka majibu yapatikane kwa watu waliokuwa wakinunua kahawa na kuwadhulumu wakuliwa. Mapunda mchapakazi, lakini ifike mahali tuache kuogopa na kufanya unafiki ungewataja waliowadhulumu wananchi wako na ungenikabidhi majina hapa leo ungeona,”

Mbunge wa Nyasa ambaye pia ni naibu waziri wa viwanda na biashara, Stella Manyanya alimwomba Rais Magufuli kuangalia namna ya kuwasaidia ujenzi wa barabara ya kutoka Tiwindi Mbambabay hadi Lituhi ambayo imekuwa changamoto kubwa kwao kutokana na uwepo wa mito mingi.