Vitambulisho vya wajasiriamali kumpa Sugu kesi ya uchochezi

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amemwagiza kamanda wa polisi, Ulrich Matei kumhoji Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa kinachodaiwa kutoa lugha zinazoonyesha kuvuruga utaratibu wake

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi almaarufu kama Sugu amewasili ofisini kwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya baada ya kupokea wito wa mahojiano.

Sugu ametii wito huo leo asubuhi, Alhamisi Februari 21, 2019 baada ya jana Kamanda Ulrich Matei kumtaka  aemde ofisini kwake.

Akizungumza na Mwananchi, Matei amesema, “Ni kweli tumemuita kwa ajili ya kumhoji kutokana na maneno yake aliyoyazungumza kuhusu vitambulisho. Maana tunaona kunakukashifu na vile ni vitambulisho vilivyotolewa na Serikali sasa tunapoona mtu anaanza kutoa maneno hayo huo ni uchochezi,” ameongeza

Kwa upande wake, Sugu amesema jana mchana alipigiwa simu na RPC Matei kwamba anatakiwa kufika ofisini kwake kwa mahojiano kwa kilichoelezwa anataka kuvuruga mchakato wa ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Rais John Magufuli.

"Nimeitwa kwa amri ya mkuu wa mkoa kuhusiana na 'clip' yangu nikiwa Iyunga na wajasiriamali waliyokuwa wakielezea changamoto ya vitambulisho.  Sasa yeye (mkuu wa mkoa) jana sijui alikuwa wapi akatangaza kuna wanasiasa wanataka kuhujumu suala la vitambulisho hivyo, ndio akaagiza polisi kuwahoji. Sasa kama kutakuwa na jingine sijui maana wamesema wanataka kunihoji," amesema Sugu.

Wakati  Sugu akizungumza na Mwananchi alikuwa tayari amekwisha kufika kituoni hapo kwa RPC.

Jana Jumatano, Chalamila akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Rungwe alisema kuna wanasiasa wanataka kukwama suala la utoaji vitambulisho hivyo na kuwataka kuacha kufanya hivyo kabla hajawachukulia hatua za kisheria.