Vituo 46,000 vya maji hoi

Dodoma. Serikali imesema kati ya vituo vya kuchota maji 131,000 vilivyojengwa kwenye maeneo ya vijijini, 46,000 havifanyi kazi.

Pia, imesema hali hiyo imesababisha upatikanaji huduma ya maji hadi Februari kuwa asilimia 64.

Akizungumza jana wakati akifungua kongamano la mwaka wa wanasayansi lililowakutanisha wafadhili na wadau wa sekta ya maji nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo, alisema watatumia kongamano hilo kueleza baadhi ya mabadiliko yaliyofanyika katika sekta hiyo.

Alisema mabadiliko hayo ni kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, ambayo imebeba mambo makubwa mawili ambayo ni uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini na muundo mpya wa jumuiya za watumiaji maji ngazi ya kijiji.

“Walikuwa wanakijiji wanakaa pale lakini sasa tumeweka mfumo wa kitaalamu. Katika jumuiya hizi kutakuwa na mtaalamu atakayehusika na sekta ya maji,” alisema.

Kuhusu upatikanaji maji, Profesa Mkumbo alisema Serikali imekuwa ikijenga vituo vya kuchotea maji maeneo ya vijijini na hadi Februari vituo 131,000 vimejengwa nchini. Alisema vituo hivyo vina uwezo wa kuhudumia watu milioni 31 na kama vituo hivyo vyote vingefanya kazi wangekuwa wameshapeleka maji vijijini kwa takriban asilimia 85.

Naye mkurugenzi wa uratibu wa Programu ya Sekta ya Maji katika wizara hiyo, Derosia Murashani, alisema kongamano hilo litahitimishwa siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji Machi 22.

“Tunashirikiana na wadau katika kutathmini huduma ya utoaji wa majisafi na usafi wa mazingira, uhifadhi, usimamizi na uendelezaji raslimali za maji nchini,” alisema.