Vuguvugu la mapinduzi laanza-3

Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume akiwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo siku chache baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Kulia kwa Karume ni Abdallah Kassim Hanga.

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi utata ulivyozidi kukua na leo tusimulia vuguvugu zilivyoanza baada ya uchaguzi uliowapa madaraka viongozi wa vyama vilivyoungwa mkono na wachache.Sasa endelea...

Leo ni siku ambayo Tanzania inasherehekea Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliuondoa utawala wa Kisultani na kuweka utawala wa wengi katika visiwa hivyo vikubwa viwili, ambavyo baadaye viliungana na Tanganyika kuunda Taifa la Tanzania. Kwa siku mbili mfululizo tumekuwa tukiwaletea makala zinazoonyesha hali ilivyokuwa katika kipindi cha kuelekea Mapinduzi hayo na jinsi vyombo vya habari vilivyojadili utata wa ushiriki wa mtu anayeitwa John Okello katika tukio hilo.

Jana tuliona jinsi utata ulivyozidi kukua na leo tusimulia vuguvugu zilivyoanza baada ya uchaguzi uliowapa madaraka viongozi wa vyama vilivyoungwa mkono na wachache.

Sasa endelea...

Pamoja na historia kutoelezea ushiriki wa John Okello katika Mapinduzi ya Zanzibar, bado taarifa za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa mtu huyo aliyekuwa raia wa Uganda ana nafasi yake katika ukombozi wa visiwa hivyo kutoka utawala wa Kisultani.

Kwa mujibu wa kitabu kinachoitwa Social Memory, Silenced Voices, and Political Struggle: Remembering the Revolution in Zanzibar kilichoandikwa na William Cunningham Bissell na Marie-Aude Fouere, Okello aliwasili Unguja akitokea Pemba na miezi kadhaa baadaye aliunda kundi la mapambano lililokuwa likikutana kwa siri.

Mganda huyo ambaye alikuwa akizungumza Kiswahili cha taabu, alikuwa akiliahidi kundi hilo kuwa kungekuwa na mabadiliko katika maisha ya watu wote wa kisiwani Unguja na Pemba kama wangeuondoa utawala wa Sultani.

Kundi hilo—kwa kuwa lilikuwa ni la watu waliokuwa na mazoea ya kufanya kazi pamoja, na nyakati nyingi wakifanya kazi ngumu katika mazingira magumu—lilikuwa tayari kufuata amri ya ‘kepteni’ au mtu yeyote aliyeonekana kuwa ‘kepteni’ ambaye alikuwa tayari kuwalipa ujira wowote.

Hayo yalifanyika wakati visiwa hivyo vikiendelea kutawaliwa na misukosuko ya kisiasa tangu kufariki kwa Sultan Khalifa. Sultani huyo alifariki Jumapili ya Oktoba 9, 1960. Sultani Khalifa alikuwa ametawala Zanzibar kwa takribani miaka 50 tangu mwaka 1911.

Waingereza walikuwa wameanza kuondoa majeshi yao, ikiwa ni pamoja na kikosi cha ziada cha Jeshi la Ireland, kilichokuwa kimeweka kambi karibu na Mji wa Mawe, lakini baadaye kiliondoka mapema mwaka 1963.

Wakati sultan mpya, Sayyid Jamshid bin Abdullah Al Said, akipandisha bendera ya ‘taifa huru’ la Zanzibar Alhamisi ya Desemba 12, 1963, kuashiria kuondoka rasmi kwa Mwingereza Visiwani Zanzibar na pia kumalizika kwa enzi ya ukoloni, haikuwa imejulikana kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja tu baadaye utawala wake ungemalizika.

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ulitoa ushindi finyu sana kwa muungano wa vyama viwili vya siasa—Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP). Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kwa mujibu wa mfumo wa utawala wa Kiingereza, kilikuwa na nafasi ndogo sana. Sultan ndiye angeonekana kama mtawala.

Lakini kumbe ushindi huo ungedumu kwa siku 33 tu. Mijadala ya kisiasa ilizidi kuongezeka na ilikuwa ya ghadhabu na maandamano ya mitaani yalianza kuonekana kama jambo la kawaida.

Mijadala hiyo ilikuwa ikihusisha makundi ya watu mitaani na ilikuwa ikitaja majina ya wanasiasa ambao wangefaa kuongoza visiwa hivyo, pia mfumo unaofaa kutumika kuendeshea taifa hilo au mfumo waliotaka utokomezwe.

Mijadala hiyo pia ilihusisha mambo kama haki dhidi ya upendeleo, wageni walioingia visiwani Pemba na Unguja kwa ajili ya kufanya kazi dhidi ya wazawa, siasa za ubepari na ujamaa, wafanyabiashara na umiliki ardhi, wananchi wa Unguja dhidi ya wa Pemba, Waasia dhidi ya Waarabu, Waswahili dhidi ya watu wa kutoka bara na mambo mengine. Maswali yalikuwa mengi kuliko majibu yake.

Okello hakuwa na majibu yoyote kwa maswali ambayo Wazanzibari walikuwa wakiuliza, lakini alikuwa na uwezo wa kutambua kwamba mambo yote hayo yaliyohusu mgongano wa masilahi yalitoa fursa nzuri sana kwa mtu wa vitendo kama yeye, kutumia nafasi hiyo kikamilifu. Isitoshe, mamia ya wanaume wachache wenye nia wangeweza kukamata vituo muhimu vya Serikali ya kisultani na vituo vitatu vikubwa vya polisi. Aliwaza kuwa mara atakapoweza kuweka vituo hivyo chini ya himaya yake na kumiliki silaha zilizohifadhiwa katika vituo hivyo, ni nani mwingine katika Unguja, au Pemba, angeweza kumwangusha?

Inaendelea kesho