Vyama sita kuchuana kumrithi Joshua Nassari

Muktasari:

Uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki unatarajiwa kufanyika Mei 19 ambapo hadi sasa vyama sita vimetangaza kushiriki ambavyo ni CCM, CUF, DP, Tadea, Demokrasia Makini na NRA

Arusha. Vyama sita vimetangaza nia ya kushiriki uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.

Uchaguzi katika jimbo hilo unatarajiwa kufanyika Mei 19 baada ya aliyekuwa mbunge, Joshua Nassari (Chadema) kupoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria vikao vitatu vya mikutano mitatu mfululizo bila kutoa taarifa.

Wakizungumza na mwananchi jana, viongozi wa vyama vya upinzani vya CUF, Demokrasia Makini, Tadea, NRA na DP walisema wapo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuteua wagombea.

Katibu wa NRA Kanda ya Kaskazini, Feruz Juma Feruz alisema watashiriki uchaguzi wa Arumeru Mashariki na mchakato wa kupata mgombea umeanza.

"Sisi tutashiriki na siku ya kwenda kuchukua fomu tume tutatoa taarifa, hivi sasa tupo katika mchakato wa kupata mgombea" alisema Feruz.

Mwenyekiti wa Demokrasia Makini mkoa wa Arusha, Simon Ngilisho alisema chama hicho kinajipanga kuhakikisha kinapata mgombea makini katika jimbo hilo.

"Tutashiriki uchaguzi na hivi sasa tupo katika mchakato wa ndani ya chama kupata mgombea" alisema.

Omar Kawaga kiongozi wa chama cha DP mkoa wa Arusha, pia alieleza chama hicho kinatarajia kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo wa Mei 19.

"Tutakuwa na mgombea katika uchaguzi huu na tunaendelea kujiandaa," alisema.

Mwenyekiti wa Tadea mkoa wa Arusha,  Fransis Ringo alisema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea na wana imani watapata mgombea mzuri ambaye atachuana na vyama vingine.

Mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa CUF, Abdallah  Shabani alisema chama hicho kinajipanga kushiriki uchaguzi huo na kipo imara kuhakikisha kinashinda.

"CUF tutashiriki uchaguzi tupo kwenye vikao vya ndani na tutatoa taarifa juu ya mgombea wetu,"  alisema.

Alisema chama hicho kitaanza kutoa fomu za kugombea Jumatatu na kinajiandaa kutoa mgombea ambaye atauzika kwa wananchi na sio mzigo.

Vyama hivyo vinatarajia kuchuana na CCM ambacho tayari kimekamilisha hatua za mwanzo za kura za maoni ndani ya chama hicho uliosimamiwa na mlezi wa CCM mkoa Arusha, Humphrey  Polepole ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM.

Katika kura za maoni, kada wa CCM, John Pallangyo alishinda kwa kupata kura 470, akifuatiwa na Dk Daniel Pallangyo kura 50,  huku William Sarakikya akipata kura 36.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza hakitashiriki uchaguzi huu.