Vyama vya siasa Tanzania vyatoa rambirambi ajali ya lori Morogoro

Muktasari:

Ajali ya lori lililokuwa limebeba mafuta ya Petroli iliyotokea Msamvu mkoani Morogoro nchini Tanzania imesababisha vifo vya watu 62 na majeruhi zaidi ya 70  ambapo vyama mbalimbali vya siasa vimetoa salamu za rambirambi kutokana na tukio hilo.

Dar es Salaam. Kufuatia ajali ya moto iliyosababishwa na lori la mafuta eneo la Msamvu Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania, vyama mbalimbali vya siasa vimetoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na tukio hilo.

Hadi saa 8 mchana wa leo Jumamosi Agosti 10, 2019  watu waliofariki katika ajali hiyo ni 62 huku zaidi ya 70 wakijeruhiwa na kulazwa hospitali ya Morogoro na wengine kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema katika taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wake wa Twitter kimezungumzia tukio hilo kikisema kupokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za awali za vyombo vya habari kuwa takriban watu 100 wameungua moto, wengi wao wamefariki dunia na wengine wengi wamejeruhiwa vibaya chanzo kikidaiwa kuwa mlipuko wa lori lililobeba petrol eneo la Msamvu, Morogoro.

Chama tawala nchini Tanzania cha (CCM), kupitia akaunti ya Twitter ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kimesema, “Uongozi wa @ccm_tanzania  umepokea kwa mshtuko taarifa za ajali ya lori huko Msamvu Morogoro ambayo imegharimu maisha ya Watanzania.”

“Rai yetu kwa Jeshi la Polisi na Zimamoto ni kuendelea kutoa elimu na kusimamia utii wa sheria. Tunatoa pole kwa wafiwa na majeruhi kupona haraka,” amesema Polepole

Taarifa ya Chama cha ACT -Wazalendo iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu amesema chama kimepokea kwa mshtuko mkubwa habari ya vifo zaidi ya watu 50.

Amesema ACT- Wazalendo kinatoa pole kwa wote waliojeruhiwa na kwa familia zilizofikwa na mauti, mwenyezi Mungu awaponye waliojeruhiwa na azilaze mahali pema roho za waliofariki.

 

Endelea  kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi