Vyombo vya habari vya kidini vyaomba kufutiwa leseni za kibiashara

Muktasari:

 

  • Vyombo vya habari za dini vimeomba kufutiwa leseni za kibiashara kwa sababu havitegemei matangazo kama ilivyo kwa vyombo vingine vya kibiashara

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Agape, Vernon Fernandes ameiomba Serikali kuvifutia vyombo vya habari vya dini leseni za uendeshaji kibiashara na badala yake kuwaweka katika mfumo usio wa kibiashara.

Ametoa ombi hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya Rais John Magufuli na viongozi wa dini ili kuzungumza masuala yanayohusu nchi.

 “TCRA wameifuta Non Commercial License wanataka sisi tufanye kazi kama ITV, EATV, tutawezaje kulipa leseni ya kibiashara wakati hatuna matangazo yanayoweza kutuingizia pesa hizo zinazotakiwa,”

Pia amesema mambo matatu yanayoweza kuikomboa nchi kiuchumi ni kilimo, madini pamoja na utalii

Amesema hata Mungu alipomuumba Adam alimuweka katika bustani ya edeni ili alime na wala sio katika ghorofa au gari.

“Mungu pia aliweka katika bustani dhahabu safi na hakuna nchi duniani ambayo ina madini safi kama Tanzania, tukiweza kusimamia eneo hili nchi itakuwa tajiri kuliko watu wanavyodhani,” amesema Fernandes.