WHO yatangaza Ebola kuwa dharura ya kimataifa

Muktasari:

Hata hivyo, WHO imeonya dharura hiyo isitumike kuwanyanyapaa au kuwaadhibu watu wanaohitaji msaada.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza ugonjwa wa ebola kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma.

Tangazo hilo la WHO limetolewa jana Jumatano Julai 18, baada ya taarifa ya kisa cha mgonjwa wa Ebola mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akitoa tangazo hilo mjini Geneva, Uswizi, Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema wakati kukiwa na uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa wa ebola nchini Congo, hatari kwa maeneo ya nje ya eneo hilo bado ni ndogo.

Hata hivyo, Ghebreyesus alionya dharura hiyo isitumike kuwanyanyapaa au kuwaadhibu watu wanaohitaji msaada.

Ghebreyesus alisema kuwa WHO haishauri kuweka vizuizi katika safari au biashara jambo ambalo badala ya kuzuia ebola, linaweza kukwamisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo.

“Kufunga mipaka kutasababisha janga kwa maisha na ustawi wa watu wanaovuka mipaka kila siku kwa ajili ya biashara, elimu au kutembelea ndugu zao.”

Awali timu ya wataalamu wa kamati ya kimataifa ya usimamizi wa afya, ilikataa kuutangaza mlipuko huo kuwa dharura ya kimataifa ingawa wataalamu wengine walisema janga hilo lina vigezo vyote vya kutangazwa.

Zaidi ya watu 1600 wameripotiwa kufa katika kipindi cha Agosti mwaka jana na Julai mwaka huu kutokana na ugonjwa huo ambao ni wa pili kwa kuua watu duniani.

Tamko la ugonjwa kuwa dharura ya kimataifa mara nyingi husaidia kuleta hamasa na kushughulikiwa zaidi kimataifa na misaada kutolewa.