Waandamanaji wazingira Ikulu Serbia kupinga hotuba ya rais

Muktasari:

Maandamano yameikumba nchi hiyo tangu Desemba mwaka jana kutokana na wafuasi wa upinzani kumtuhumu Rais kuwa anaielekeza nchi kuwa ya kidikteta.

Belgrade, Serbia. Maelfu ya wandamanaji leo wamezingira makazi ya Rais wa Serbia jijini Belgrade kupinga hotuba ya Rais Aleksandar Vucic ya kupuuza maandamano hayo na kuwaita wahuni, ikiwa ni siku moja baada ya wafuasi wa vyama vya upinzani kuvamia kituo cha televisheni inayomilikiwa na serikali.
Hatua hiyo inaashiria mwamko mpya wa ujasiri wa wafuasi wa vyama vya upinzani katika kufanya maandamano, ambayo yamekuwa yakifanyika kila wiki kuanzia Desemba kupinga hatua za rais huyo ambazo wanaona zinaielekeza nchi kuwa ya utawala wa kidikteta.
Jumamosi usiku, mamia ya waandamanaji walivamia ofisi za televisheni ya RTS, ambayo waandamanaji wanaituhumu kuwa inapendelea chama tawala wakiitaka kuzungumzia maandamano yao na kuyarusha moja kwa moja.
Viongozi wa vyama vya upinzani wameanza kuonekana bayana kwenye maandamano hayo, na miongoni mwa waliovamia RTS ni pamoja na meya wa zamani wa Belgrade, Dragan Djilas na kiongozi wa chama cha Dveri, Bosko Obradovic.
Katika maandamano ya leo Jumapili, polisi wa kutuliza ghasia, ambao awali walikuwa hawaonekani sana katika maandamano hayo ambayo kwa kawaida huwa ya amani tangu yalipoanza Desemba 8, walizuia waandamani kuingia karibu na eneo ambalo Vucic alitaka kuzungumza, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP.
Katika hotuba yake aliyoitoa akiwa Ikulu na iliyorushwa moja kwa moja na RTS, Vucic alisema hatishwi na maandamano hayo na kuwaita waandamanaji kuwa ni wahuni.
Pia aliwashutumu viongozi wa upinzani, akimuita Obradovic "fashisti".
Vucic amekanusha kuwa amebadilika na kuwa dikteta.
Serbia, ambayo inataka kujiunga na Umoja wa Ulaya ifikapo mwaka 2025, ilikosolewa na jumuiya hiyo mwaka jana wakati wa siku ya uhuru wa habari, kutokana na kuwatisha na kuwakamata waandishi wa habari.