Wabunge 28 wa CUF Maalim njia panda

Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba aki-pongezana na Makamu Mwenyekiti Bara, Nachuma Maftah. Kulia ni Makamu Mwenyekiti, Zanzibar, Abass Juma Muhunzi. Picha na Anthony SiameMGOGORO

Dar es Salaam/Zanzibar. Kupatikana kwa uongozi mpya wa CUF ni kama vile unawaweka njia panda wabunge 28 na viongozi wa upande wa Zanzibar waliojinasibu kumuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad.

Tegemeo pekee kwao ni uamuzi wa Mahakama Kuu unaotarajiwa kutolewa leo kuhusu shauri la uhalali wa uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Jumla ya wabunge 28 wa CUF walitangaza kuendelea kumuunga mkono Maalim Seif na kujitenga na Profesa Lipumba, lakini hatma yao sasa itakuwa mikononi mwa Profesa Lipumba, ambaye bado uhalali wake kuendelea kukalia kiti unasubiri uamuzi wa mahakama.

Profesa Lipumba alisababisha mgawanyiko ndani ya chama hicho baada ya kujiuzulu uenyekiti na kukaa nje kwa mwaka mmoja kabla ya kurudi na kutaka kuhudhuria Mkutano Mkuu, akidai kuwa amerejea kwenye nafasi yake kwa kuwa CUF haikukaa kuridhia kujiuzulu kwake.

Maalim Seif na wenzake walipinga, lakini Msajili wa Vyama vya Siasa akatoa barua ya kuhalalisha kurejea kwake na hivyo kuibuka mgawanyiko, huku kundi la Lipumba likishikilia ofisi za makao makuu zilizo Buguruni.

Mpasuko huo uliwafanya wabunge hao kutafuta ofisi eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

Katika Uchaguzi wa 2015, CUF ilipata jumla ya wabunge 42, kati yao wa majimbo ya Tanzania Bara na Zanzibar walikuwa 32 na viti maalumu 10.

Hata hivyo, wabunge watatu wa Bara walihamia CCM.

Wabunge 28 wa majimbo kati yao 22 kutoka Zanzibar na wanne wa Bara na mmoja wa viti maalumu wameonekana kuwa na Maalim Seif. Wakati wabunge watatu wa majimbo ya Bara na tisa viti maalumu kwa Lipumba.

Tayari Profesa Lipumba na wenzake wameshabadili katiba inayompa mamlaka ya kuteua katibu mkuu, ambaye sasa ni Khalifa Suleiman Khalifa akichukua nafasi ya Maalim Seif.

Baadhi ya wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif walikuwa na kauli tofauti walipoulizwa na gazeti hili kuhusu mustakabali wao.

“Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa hadi hukumu ya mahakama itoke,” alisema mbunge wa Tandahimba, Ahmad Katani.

Kwa upande wake, mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara pia alisema anaheshimu uamuzi wa Mahakama Kuu uliozuia mkutano mkuu wa CUF.

“Sina mengi ya kusema, lakini kwa akili yangu nina heshimu uamuzi uliotolewa kuhusu mkutano mkuu,” alisema.

Wakati wabunge hao wakieleza hayo, katibu mkuu mpya alisema CUF haiwezi kujenga chuki na baadhi ya wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif kwa sababu ni wabunge wa chama hicho waliochaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Lakini, watambue siku si nyingi tutawaita ili tuzungumze nao. Wale watakaonyesha kuwa na mwelekeo na upande fulani, tutawachukulia hatua na wale watakaokuwa bega kwa bega na chama tutakuwa nao sambamba maana tunawajua,” alisema Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando.

Hatua ambayo CUF inaweza kuichukua ni kuwavua uanachama na hivyo kupoteza sifa ya kuwa wabunge. Lakini katika chaguzi zote ndogo zilizofanyika mwaka jana, CCM ilishinda isipokuwa kata moja ya mkoani Mbeya ambako Chadema ilishinda udiwani.

Akionekana kutambua hilo, mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk alishauri wabunge hao kurudi ndani ya chama ili kukijenga na kukiimarisha na kwamba hivi sasa si wakati wa kumfuata mtu.

“Mimi nilikuwa namuunga mkono Maalim Seif, lakini niliangalia upepo na kwa sasa nipo upande wa Lipumba,” alisema.

“Nawaambia wenzangu chama kimeshapata viongozi wapya na Maalim Seif si kiongozi tena warudi tuijenge CUF.”

Naye Nassor Ahmed Mazrui, ambaye upande wa Maalim Seif unamtambua kuwa ni naibu katibu wa Zanzibar, alisema bado anaendelea na wadhifa wake na mabadiliko yaliyofanyika hayatambui kwa kuwa ni haramu. “Siwezi kufanya kazi na wao,” alisema.