Wabunge 7 Chadema kuvuliwa nyadhifa

Arusha. Hali si shwari ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini baada ya kamati ya utendaji ya chama hicho kupendekeza kwa kamati kuu kuvuliwa nafasi za uongozi wa chama wabunge saba na kuvuliwa uanachama meya mmoja wa jiji kutokana na makosa ya kinidhamu.

Kamati hiyo pia imemvua uanachama Diwani Viti Maalumu Chadema katika jimbo la Arumeru Mashariki, Digna Nassari kwa tuhuma ya makosa ya kinidhamu na usaliti.

Akizungumza mjini hapa jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema chama hicho kina wabunge 14 na mameya wawili Kanda ya Kaskazini ambao baadhi wanashika nyadhifa za chama ikiwapo ujumbe wa kamati kuu, mawaziri vivuli na nafasi nyingine kadhaa.

Akitangaza uamuzi wa kikao cha kamati ya utendaji kilichofanyika Mei 18, mwaka huu na kuongozwa na kaimu mwenyekiti ambaye ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Golugwa alisema wamechukuwa uamuzi huo ili kukisafisha chama kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Hata hivyo, Golugwa aliomba kutotaja majina ya wabunge wanaopendekezwa kuvuliwa nyadhifa zao.

Alisema tuhuma ambazo zimewatia hatiani viongozi hao ni kukaidi na kutoshiriki kazi za chama ambazo zinahitaji wao kutumia hadhi, heshima na uwezo wao ili kukijenga.

Golugwa alisema viongozi hao pia wametiwa hatiani kwa kukaidi maelekezo ya chama kuhusiana na michango yao kwa ajili ya ujenzi wa chama na utekelezaji wa maeneo waliyopangiwa ya kikazi ya Chadema. “Viongozi hawa pia wametiwa hatiani kwa kukaidi kufika kweye vikao vya chama bila taarifa yoyote” alisema.

Alidai baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakitoa lugha kwenye mikutano ya hadhara zinazokinzana na msimamo wa chama hicho.