Wabunge Democratic wamjibu Rais Trump

Tuesday July 16 2019

 

Washington, Marekani. Wabunge wa Chama cha Democratic wasiyo na asili ya Marekani wamepuuza tamko la Rais Donald Trump la kuwataka waondoke nchini humo.

Aidha wabunge hao wamesema kiongozi huyo ana lengo la kuwakandamiza na kuwanyamazisha hivyo hawatokubali hilo litokee.

Tamko la wabunge hao limekuja siku chache baada ya utawala wa Rais, Trump kutangaza kuanza kwa utekelezaji wa operesheni ya kuwaondoa watu wasiyo na vibali vya kuishi nchini humo.

Kupitia akaunti yake ya twitter, Rais Trump alisema kampeni hiyo inalenga kuwafuatilia watu wote walio na amri za mwisho za kurejea katika nchi zao, zikiwamo familia za wahamiaji ambazo kesi zao zilikuwa zikifutiliwa kwa haraka na majaji katika majiji 10.

Rais Trump pia aliwageukia wabunge hao wanawake wanaotoka chama cha Demoratic na kudai kuwa “wabunge hao wamewasili kutoka mataifa ambayo serikali zake ni majanga matupu hivyo ni bora warudi walikotoka.”

Lakini jana mmoja wa wabunge hao, Ilhan Omar alisema “kikosi chetu ni kikubwa, kinahusisha mtu yeyote aliye tayari kujenga ulimwengu wa usawa na haki,”

Advertisement

Wabunge hao walisema kuwa maneno ya Trump yanadhihirisha kuwa mashambulizi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya wanawake yenye lengo la kuigawa nchi.

Wabunge hao ni pamoja na Alexandria Ocasio-Cortez, Rashida Tlaib na Ayanna Pressley walizaliwa na kulelewa nchini Marekani na Ilhan Omar ambaye alihamia nchini Marekani alipokuwa mtoto.

Advertisement