Wabunge walalamikia tani 1,500 za mafuta kukwama bandarini

Muktasari:

  • Hadi sasa mzigo wa mafuta ya kula uliopo bandarini ni tani 1,500 ambazo zimekaa kwa zaidi ya miezi saba kutokana na mgongano wa uamuzi baina ya mamlaka za udhibiti juu ya vipimo vilivyobainisha aina ya mafuta yanayoingizwa

Dodoma. Wabunge wamesema hadi sasa mzigo wa mafuta ya kula uliopo

bandarini ni tani 1,500 ambazo zimekaa kwa zaidi ya miezi saba kutokana na mgongano wa uamuzi baina ya mamlaka za udhibiti juu ya vipimo vilivyobainisha aina ya mafuta yanayoingizwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana Jumanne Mei 14, 2019 bungeni na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Kanali mstaafu Masoud Ali Khamis wakati akisoma maoni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya 2019/20.

Alisema mahitaji ya mafuta nchini ni tani 700,000 na uzalishaji wa bidhaa ni tani 210,000 na kwamba, tofauti iliyopo iruhusiwe kuingia kutoka nje ya nchi.

Alisema hali hiyo ilisababisha ucheleweshaji wa kutoa mafuta bandarini na kuongeza gharama za uhifadhi.

“Kamati inashauri Serikali kuzisimamia kwa ukaribu mamlaka hizo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi mapana ya nchi,” alisema.

Kuhusu sukari, Khamis alisema sekta hiyo imegubikwa na malalamiko juu ya viwango vya sukari inayoingia nchini ukilinganisha na mahitaji halisi.

“Kamati inashauri Serikali kuweka umakini mkubwa wakati wa kutoa vibali vya kuingiza sukari nchini na kuwa vibali vitolewe baada ya Serikali kufanya tathmini na kubaini upungufu wa sukari

uliopo,” alisema.

Kanali Khamis alisema malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) ambayo hayajarejeshwa kwa wahusika, hivyo katika mwaka 2018/19 kufikia Sh45 bilioni.

“Kamati inatambua mchakato wa uhakiki uliokuwa unaendelea kufanyika lakini kamati inashauri kukamilishwa kwa mchakato huo na kuanza kurudisha fedha hizo kwa wahusika,” alisema.

Akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa wizara

Hiyo, Cecil Mwambe alisema mchakato wa kupata vibali vya kufanyia kazi

nchini kwa waajiriwa kwenye sekta mbalimbali ni changamoto kubwa

pamoja na matamko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na idara ya

kazi.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri Serikali kuhakikisha inarahisisha mchakato wa kuomba vibali vya ajira nchini kufanywa kwa njia ya mtandao yaani online ili kuondoa ukiritimba uliopo na kuharakisha mchakato wa uamuzi huo,” alisema.

Kuhusu mazingira ya uanzishwaji wa biashara nchini, Mwambe alisema

mazingira ya kuanzisha biashara nchini ni magumu.

Alisema kuanzisha biashara ya kawaida unaweza kutakiwa kupitia kwenye

mamlaka na wakala zaidi ya tano na sehemu hizo zote kuna gharama

ambazo lazima uzilipe kama mfanyabiashara kupata vibali au utendaji.

Pia, alisema utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) sio rafiki kwa

wafanyabiashara wana hofu na kuamua kufunga biashara zao.