Wabunge walia barabara za majimboni

Mbunge wa Momba, David Silinde akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma juzi. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Suala la kutokamilika kwa miradi ya ujenzi wa barabara linaonekana kutamalaki mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano, ikiwa ni takriban mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wabunge wengi waliochangia mjadala huo Alhamisi na Ijumaa iliyopita, walielekeza hoja zao katika barabara zilizo majimboni mwao, ambazo zinaweza kuwa turufu katika kampeni zao mwakani.

Mbunge wa Muheza (CCM), Adadi Rajabu alisema katika jimbo lake hasa barabara ya Amani - Muheza yenye urefu wa kilomita 36 imekuwa inatengewa fedha tangu mwaka juzi, lakini haijajengwa. Alisema mwaka 2017 ilitengewa Sh3 bilioni, mwaka jana Sh5 bilioni na mwaka huu Sh2 bilioni.

”Lakini tatizo ambalo lipo ni la mkandarasi kuwa pale. Najua meneja Tanroads (wa mkoa wa Tanga, Alfred) Ndumbaro anafanya juu - chini, lakini kila ukimuuliza anakuambia ‘hapana bado kidogo kuna mchakato wa mzabuni’,” alisema Adadi ambaye kabla ya kuwa mbunge 2015, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga alizungumza huku akitetemeka sauti sauti kwa kulia.

“Nimetuma kwenye magrupu ya Bunge, nimemtumia waziri, kama kijiko kinazama barabara ya kutoka Ifakara hadi Mlimba hivi akinamama wa kutoka Mlimba wataendaje Ifakara kujifungua?” alihoji huku akilia.

Alisema barabara hiyo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu tangu 2017, lakini haijengwi kwa kiwango cha lami na kumuomba Waziri Isack Kamwelwe ili itengenezwe.

“Hivi wananchi wanaoishi Mlimba mnawahesabu katika kundi gani nchi hii? Hali mbaya. Kama ni hali ya dharura, ipo Mlimba,”

Alisema mkandarasi akipewa mkataba wa kuhudumia barabara hiyo mwakani haonekani.

Kilio kama hicho kilitolewa na mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Mary Chatanda aliyesema barabara ya Old Korogwe hadi Soni ilianza kuzungumziwa na aliyekuwa mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani ‘Profesa Majimarefu’ na pia iliwekwa katika Ilani ya uchaguzi, lakini bado haijajengwa. Majimarefu alifariki dunia Julai 2, 2018.

“Naomba sasa huu upembuzi yakinifu ukafanye kazi. Sasa ni miaka 10 barabara hii inafanyiwa upembuzi yakinifu tu. Hata watu wa mlimani wanahitaji barabara za lami. Nimuombe waziri fedha hizi zitoke,” alisema.

Mbunge mwingine aliyezungumzia barabara za jimbo lake ni Willy Qambalo wa Karatu (Chadema).

Qambalo alisema wameiongelea kwa muda mrefu barabara ya Karatu - Mbulu hadi Hydom na kwamba zimetengwa Sh1.4 bilioni.

“Hizi fedha zitakwenda kufanya nini ambazo nadhani wakati mwingine mnaturidhisha tuone kuwa vitu vimeandikwa, lakini hakuna kitu unaweza kufanya. Kule zimetegeshwa tu,” alilalamika mbunge huyo.

“Na hizi ni kwa ajili ya kujenga lami ama kuendelea na upigaji uleule wa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na mambo mengine?”

Lakini mbunge wa Magu (CCM), Boniventura Kiswaga alilalamikia kutokamalika kwa miradi kutokana na kukwamishwa na sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa za ujenzi.

Mjadala wa bajeti hiyo utahitimishwa kesho kwa mawaziri kujibu hoja za wabunge.