Wabunge waliokuwa kwa Maalim Seif, waanza kurejea kwa Lipumba

Muktasari:

Baadhi ya wabunge waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad akiwemo Bobali wameanza kujerea wakisema ni wakati wa kuijenga CUF


Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad akiwemo Hamidu Bobali wa Mchinga wameanza kumuunga mkono mwenyekiti wa hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Bobali ametangaza uamuzi wa kumuunga mkono Profesa Lipumba leo Jumanne Machi 19, 2019 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za makao makuu ya Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Amesema wapo wengi watakaorudi kuungana na Profesa Lipumba na kusema hivi sasa ni wakati wa kukijenga chama hicho na walioondoka kwenda sehemu nyingine ni utashi wao.

"Nimerudi nyumbani baada ya msuguano uliodumu kwa miaka mitatu ndani ya CUF na uliokidhoofisha chama, nawaomba mnisamehe kwa yaliyotokea," amesema Bobali.

"Najua kuna wenzangu wanataka kurudi lakini wanashindwa wataanzia wapi, nawaambia mimi nimeonyesha njia waje wasiogope wakati ndio huu," amesema .

Kwa upande wake, Profesa Lipumba amesema hawana nia ya kuwafukuza uanachama wabunge hao bali wanataka nidhamu ndani ya CUF na wameshaandikia barua wakitaka kurejea.

Bobali amechukua uamuzi huo wakati leo Jumanne Maalim Seif pamoja na viongozi mbalimbali waliokuwa CUF wamekabidhiwa kadi za uanachama wa ACT- Wazalendo.

Maalim Seif jana Jumatatu wakati akitangaza uamuzi wa kujiunga na ACT-Wazalendo alisema wamewaacha wabunge waamue wenyewe kama watamfuata au watabaki ndani ya chama hicho.